TANGAZO

TANGAZO

TANZANIA YAONGOZA MJADALA WA KIMATAIFA KUHUSU UIMARISHAJI WA HUDUMA NA UWEZESHWAJI KWA WATU WENYE ULEMAVU







Na.mwandishi wetu- New York, Marekani


Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Togolani Mavura, ameongoza mjadala wa ngazi ya juu katika Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19), uliojikita katika mada ndogo ya “Jamii Imara: Kuimarisha Mifumo ya Huduma na Msaada ili Kuhakikisha Uwezeshaji, Uhuru na Kujitegemea kwa Watu Wote Wenye Ulemavu.”





Akifungua mjadala huo, Mhe. Balozi Togolani  amesema huduma na mifumo ya msaada ni msingi muhimu wa ustawi wa watu binafsi, jamii na uchumi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu umeleta mafanikio makubwa duniani katika kipindi cha miaka 20 tangu kupitishwa kwake.


"licha ya hatua zilizofikiwa, bado watu wengi wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto za kupata huduma na msaada unaokidhi mahitaji yao, hali iliyodhihirika zaidi wakati wa janga la UVIKO-19 ambapo mifumo mingi ya huduma ilionekana kutokuwa imara na jumuishi vya kutosha hivyo ni muhimu  kuimarisha huduma za usaidizi binafsi, huduma za urekebishaji na uendelezaji uwezo, vifaa saidizi, mifumo ya hifadhi ya jamii pamoja na huduma za kijamii zinazotolewa katika ngazi ya jamii katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kufanya maamuzi yao wenyewe, kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa."Alisema Mhe. Balozi Togolani.


Aidha, amesema kuwa uwekezaji katika mifumo ya huduma na msaada si suala la maendeleo pekee bali ni wajibu wa kuheshimu haki za binadamu, huku akizitaka serikali, mashirika ya maendeleo, asasi za kiraia, mashirika ya watu wenye ulemavu na wadau wengine kushirikiana kwa karibu ili kuziba mapengo yaliyopo na kuharakisha utekelezaji wa sera na programu zinazolenga kujenga jamii jumuishi na himilivu.


Kwa upande wake Afisa  Sheria kutoka kitengo cha  Watu Wenye Ulemavu,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Bw. Jacob C. Mwinula, akiwasilisha uzoefu wa Tanzania katika kuimarisha mifumo ya huduma na uwezeshwaji kwa watu wenye ulemavu wakati wa mjadala (Roundtable Discussion) ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ujumuishaji, kujitegemea na ushiriki wa watu wenye ulemavu kupitia sera, sheria, mifumo ya hifadhi ya jamii, huduma za afya, elimu jumuishi na uwezeshaji wa kiuchumi.