-Wajionea miradi ya umeme vitongijini inavyotekelezwa kwa ufanisi
Watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoka nchini Zambia wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Alex Mbumba, wametembelea Kitongoji cha Vikonje A na Shule ya Msingi Chahwa, wilayani Chamwino mkoani Dodoma ambapo wamejionea namna Tanzania inavyotekeleza miradi ya umeme vijijini na vitongojini na jinsi miradi hiyo inavyochochea shughuli za kijamii na kiuchumi.
Ziara hiyo imefanyika Juni 24, 2026 ikiwa ni sehemu ya programu ya kubadilishana uzoefu kati ya REA Tanzania na REA Zambia hususan mbinu bora za utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuongeza manufaa ya nishati kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo, Bw. Mbumba amesema ziara hiyo imekuwa fursa muhimu ya kujifunza muundo wa taasisi ya REA Tanzania, kubadilishana uzoefu wa kiufundi na kujionea jinsi miradi inavyotekelezwa kwa ufanisi.
“Moja ya jambo kubwa tunalojifunza hapa ni kwamba sote tuna lengo linalofanana. Tunataka nishati ya umeme isiishie kuwa huduma ya kijamii pekee, bali iwe chombo cha kuchochea shughuli za kiuchumi katika jamii tunazozihudumia,” amesema Bw. Mbumba.
Kwa upande wake, Meneja Msimamizi wa Miradi ya Umeme Vijijini kutoka REA Tanzania Mhandisi Deogratius Nagu, amesema miradi ya umeme vijijini imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii.
Ameeleza kuwa pamoja na kuwezesha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, umeme pia unasaidia sekta ya elimu ambapo wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wao kutokana na upatikanaji wa nishati ya uhakika.


