TANGAZO

TANGAZO

MHE. KILAKALA AIPONGEZA WIZARA YA NISHATI KWA KUENDELEA KUTOA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


 



Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kuandaa Warsha ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wanahabari na Maafisa habari, akisema mafunzo hayo ni hatua muhimu ya kuhakikisha elimu sahihi inawafikia wananchi na kuimarisha utekelezaji wa ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.





Akizungumza Julai 15, 2026 wakati wa ufunguzi wa Warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari, Maafisa Mawasiliano Serikalini wa Mikoa, Taasisi, Wizara pamoja na Taasisi zilizo  chini ya Wizara ya Nishati kuhusu uandishi na uhamasishaji wa masuala ya nishati safi ya kupikia inayofanyika katika Ukumbi wa Morena Hotel mkoani Morogoro amesema Mkoa wa Morogoro una vyanzo vingi vya maji vinavyopaswa kulindwa, hivyo ajenda ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia itasaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti, kulinda afya za wananchi pamoja na kutunza vyanzo hivyo vya maji kwa manufaa ya kizazinkijacho.


Amesema elimu inayotolewa kupitia warsha hii ikiwafikia wananchi kwa usahihi, itasaidia kuongeza uelewa kuhusu maana na faida za nishati safi ya kupikia, hususan kwa jamii za vijijini, jambo litakalowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za kulinda mazingira na kutumia nishati salama na nafuu.


Mhe. Kilakala amewataka washiriki kutoka Mikoa mbalimbali nchini kutumia maarifa waliyoyapata katika warsha hiyo kwa weledi mkubwa wanaporejea kwenye maeneo yao ya kazi kwani mafunzo haya yataongeza hamasa na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na elimu ya nishati safi ya kupikia na hivyo kuchangia kufikiwa kwa malengo ya taifa ya kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.