TANGAZO

TANGAZO

QATAR YAFUNGUA FURSA MPYA YA AJIRA KWA WATAALAM KUTOKA TANZANIA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu (katikati) akiwa ameambatana na ujumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika majadiliano na Viongozi wa Taasisi ya Serikali ya Qatar inayosimamia huduma za Ajira (JUSOUR), Jijini Doha, Nchini Qatar tarehe 7 Julai, 2026.


Zaidi ya vijana 9,500 wa Kitanzania wameunganishwa na fursa mbalimbali za ajira ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miezi sita iliyopita, huku ushirikiano mpya kati ya serikali ya Tanzania na Qatar ukitarajiwa kufungua milango mikubwa zaidi ya kazi kwa wataalamu wa kada mbalimbali.

Kada hizo ni pamoja na afya, uhandisi, TEHAMA na wahadhiri wenye Shahada za Uzamivu (PhD). 

Hatua hii kubwa na ya kimkakati imefikiwa kufuatia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira Tanzania (TRAA) na Taasisi ya Serikali ya Qatar inayosimamia huduma za ajira (JUSOUR). 

Makubaliano haya yanarahisisha mfumo kwa Watanzania kuomba ajira moja kwa moja, huku waajiri kutoka Qatar wakiratibu usaili na kutoa mikataba yenye maslahi bora kwa wafanyakazi.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi mjini Doha Julai 7, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amebainisha kuwa ushirikiano huo umeendelea kuzaa matunda tangu mataifa hayo mawili yaliposaini makubaliano ya awali ya ajira mwaka 2018. 

Kupitia diplomasia ya uchumi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, soko la kazi la Qatar limekuwa mkombozi mkubwa kwa nguvu kazi ya Tanzania. 

Waziri Sangu amepongeza weledi, uadilifu, bidii na nidhamu ya juu inayojitokeza kwa vijana wa Kitanzania waliopo nchini humo, jambo lililojenga imani kubwa kwa Serikali ya Qatar na kuifanya itafute njia za kupanua zaidi wigo wa ushirikiano huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu (katikati) akishuhudia zoezi la utiaji saini wa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kuhusu masuala ya ajira za kitaalamu kati ya Chama cha Wakala Binafsi wa Ajira Tanzania (TRAA) na Taasisi ya Serikali ya Qatar inayosimamia huduma za ajira (JUSOUR) iliyopo chini ya Wizara ya Kazi ya Qatar, tarehe 7 Julai, 2026.


Katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ofisi ya Waziri Mkuu imejikita kuendelea kutafuta masoko mapya ya ajira duniani kote ili kuwasaidia vijana. 

Waziri Sangu ameishukuru serikali ya Qatar kwa kuboresha sheria zake za kazi zinazolinda haki za wafanyakazi wa kigeni na kuweka adhabu kali kwa waajiri wanaokiuka taratibu. 

Upande wake, Mwenyekiti wa TRAA, Abdallah Mohamed, amethibitisha kuwa ushirikiano huu unazidi kupanua wigo wa ajira. 

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania pia ulitembelea chuo maalumu cha mafunzo ya wahudumu wa watoto wanaohudumia familia za kifalme nchini Qatar, ambapo tayari vijana 77 wa Kitanzania wamepata mafunzo kwa ufadhili na kuajiriwa, huku wengine 20 wakitarajiwa kujiunga na programu hiyo hivi karibuni baada ya kukamilisha taratibu zilizobaki.