TANGAZO

TANGAZO

TIANPIN YAOMBA RADHI, YAAHIDI MABADILIKO YA HARAKA, SERIKALI YASISITIZA ULINZI KWA WAFANYAKAZI

Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda akizungumza na Meneja wa kampuni ya TIANPIN Investment Management Ltd Yin Yanqiang (kulia) wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa wilaya.

Na Neema Nkumbi, Kahama


Kampuni ya Tianpin Investment Management Ltd imeomba radhi kwa kasoro zilizobainika katika mgodi wake uliopo kijiji cha Mhandu, kata ya Segese wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, huku ikiahidi kufanya mabadiliko ya haraka ndani ya siku saba kwa kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Serikali kuhusu ulinzi wa haki na maslahi ya wafanyakazi.

Hatua hiyo imekuja baada ukaguzi uliofanywa na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kahama iliobaini ukiukwaji wa sheria za kazi, madini na mazingira katika mgodi huo.

Ahadi hiyo imetolewa na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo nchini (Country Manager), Yin Yanqiang, alipofika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, kueleza hatua ambazo kampuni imeanza kuzichukua ili kutekeleza maelekezo ya Serikali.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Nkinda amesema ukaguzi wa kamati hiyo ulibaini changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi wa Kitanzania kutokana na kutokuzingatiwa kwa sheria za kazi na madini.

"Tumepokea ugeni kutoka kampuni ya Tianpin baada ya ukaguzi tulioufanya na kubaini changamoto mbalimbali ambazo Watanzania walikuwa wanakumbana nazo kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa kampuni dhidi ya sheria zetu za kazi na madini," amesema.

Amesema Serikali iliipa kampuni muda wa siku saba kutekeleza matakwa yote ya kisheria, huku Kamati ya Usalama ikitarajiwa kurejea mgodini baada ya muda huo kujiridhisha na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa.

"Baada ya siku saba Kamati ya Usalama itarudi tena kujiridhisha juu ya utekelezaji wa ahadi walizotoa za kutekeleza matakwa ya kisheria ambayo kwa kiasi kikubwa hayakuwa yametekelezwa," amesema.

Kwa upande wake, Yin amesema aliporejea katika kampuni yake baada ya kutokuwepo wakati kasoro hizo zikibainika, aliona ni muhimu kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuthibitisha dhamira ya kampuni ya kushirikiana na Serikali na kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa.

"Ninaahidi tutatekeleza yote tuliyoelekezwa, Tutahakikisha wafanyakazi wote wanapata mikataba ya ajira, vifaa vya kujikinga kazini na muda wa kutosha wa kupumzika, Pia wafanyakazi wa Kichina lazima waheshimu watu wa eneo hili," amesema.

Ameongeza kuwa kampuni imepanga kukamilisha marekebisho yote ndani ya siku saba kuanzia Julai 14, 2026, huku akiomba radhi kwa kasoro zilizojitokeza.

"Ninaomba radhi kwa mambo yote yaliyotokea, Kampuni yetu itabadilika, na nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kila kitu kinakuwa vizuri," amesema.

Akihitimisha, Nkinda amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, lakini akaweka wazi kuwa uwekezaji lazima uende sambamba na kuheshimu sheria za Tanzania, kulinda haki za wafanyakazi na kuhakikisha mazingira salama ya kazi.

"Tunawajibika kuwalinda wawekezaji wetu ili waendelee kukua, lakini wakati huohuo tunawajibika kuwalinda Watanzania wanaofanya kazi katika maeneo hayo ili kuimarisha imani yao kwa Serikali," amesema Dc Nkinda.