TANGAZO

TANGAZO

SERIKALI YAOKOA WAATHIRIKA 160 WA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU, WATUHUMIWA 57 WAKAMATWA


Serikali imeeleza mafanikio yake makubwa katika mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu kwa kuokoa waathirika 160 na kuwakamata watuhumiwa 57 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026, ikionyesha jinsi inavyoendelea kuimarisha ulinzi kwa wananchi wake. 

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu yenye kauli mbiu "Jihadhari na Utumwa Kupitia Utapeli Mitandaoni", Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alibainisha kuwa kati ya waathirika hao, 126 waliokolewa wakiwa ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa, huku 34 wakirejeshwa kutoka mataifa ya nje, na kati ya watuhumiwa waliokamatwa, 45 tayari wamefikishwa mahakamani huku 12 wakiwa kwenye hatua za uchunguzi na upelelezi.

Katika kuimarisha hatua za kuzuia na kutoa msaada, serikali imechukua hatua madhubuti ikiwemo kuanzisha kituo cha kupokea taarifa kupitia namba ya bure 195 inayomwezesha kila Mtanzania kutoa taarifa za uhalifu huo, kuanzisha mfuko maalum wa kuwasaidia waathirika, na kutoa elimu kwa wananchi zaidi ya elfu 19. 

Aidha, serikali inajenga nyumba salama inayolenga kulinda na kutoa afua kwa waliokumbwa na kadhia hiyo, ujenzi ambao umefikia asilimia 73 na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2026.

Mafanikio haya na jitihada za serikali zilionekana wazi kupitia ushuhuda wa kusisimua kutoka kwa mmoja wa manusura, aliyeeleza jinsi alivyodanganywa na kuchukuliwa hadi Zanzibar kusaini mkataba kabla ya kusafirishwa kwenda Oman, ambako baada ya mwezi mmoja ratiba ilibadilika na kuanza kukumbana na mateso makubwa na unyanyasaji wa kingono. 

Manusura huyo alieleza jinsi awali alivyokuwa anailaumu serikali, lakini sasa anaishukuru sana kwa upendo na moyo wa kujali wananchi wake baada ya kuokoa maisha yake na kumrejesha salama nyumbani nchini Tanzania.