Serikali imewasilisha rasimu ya Mwongozo wa Uratibu wa Mahusiano baina ya Serikali na Makundi ya Kijamii wa mwaka 2026 kwa wadau mbalimbali ili kupokea maoni na ushauri wao wa mwisho kabla ya mwongozo huo kukamilishwa rasmi na kutolewa kwa umma.
Akizungumza katika warsha maalum jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Maganga,Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano, Bw. Rasheed Maftah ameeleza kuwa mwongozo huo ni nguzo kuu itakayofanya kazi kama daraja la mawasiliano na ushirikishwaji wa dhati kati ya serikali na wananchi, ikihakikisha kuwa sauti na maoni ya wadau yanazingatiwa kikamilifu katika maamuzi yanayohusu masuala ya kitaifa.
Aidha Maftah alisema hatua hiyo ya kuwashirikisha wadau inakuja kufuatia jukumu jipya lililokabidhiwa ofisi hiyo mnamo Novemba 2025 la kuratibu mahusiano baina ya serikali na makundi mbalimbali yakiwemo vyama vya siasa, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, na asasi za kiraia.
“Kama mnavyofahamu, Novemba 2025, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ilipewa jukumu jipya la kuratibu suala la mahusiano baina ya Serikali na makundi ya kijamii, ikiwemo vyama vya siasa, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia,” amesema Maftah.
Maftah ameeleza kuwa baada ya kupewa jukumu hilo, Ofisi imekutana na makundi mbalimbali kwa nyakati tofauti kwa lengo la kulitambulisha jukumu hilo, kuelimishana kuhusu dhana ya mahusiano na ushirikishwaji, pamoja na kupokea maoni kuhusu namna bora ya kuimarisha mahusiano baina ya Serikali na makundi ya kijamii. Maftah amesisitiza kuwa maoni hayo yamezingatiwa katika uandaaji wa rasimu ya mwongozo.
Aidha Maftah amefafanua kuwa mwongozo huo si wa Serikali pekee, bali ni wa manufaa kwa makundi yote ya kijamii, yakiwemo vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini, asasi za kiraia, wazee, vijana, wanawake na makundi mengine muhimu katika jamii na kutaka wadau wote kushiriki kutoa maoni.
“...ni wajibu wetu sote kushiriki katika kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yatakayoboresha mwongozo huu na kuhakikisha unatekelezwa kwa vitendo kwa ajili ya manufaa ya taifa letu,” alisema Maftah.
Kupitia mwongozo huu, serikali inalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji wa pamoja, na kujenga misingi thabiti ya usawa, maadili, na mshikamano wa kitaifa, huku ikihakikisha kuwa hati hiyo haibaki kuwa ya serikali pekee bali inakuwa mali na manufaa kwa makundi yote ya jamii pamoja na wazee, vijana, na wanawake.
Manufaa ya uwepo wa mwongozo huu ni pamoja na kuondoa migongano ya kimawasiliano, kuleta uelewa wa pamoja wa dhana ya ushirikishwaji, na kutoa fursa kwa wananchi kuwa sehemu ya uendeshaji wa serikali kupitia njia zilizopangwa.
Wadau mbalimbali waliohusika katika warsha hiyo, wakiwemo viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini, na jumuiya za maridhiano, wameipongeza serikali kwa kuwatambua na kuwashirikisha tangu hatua za awali, wakisisitiza kuwa mfumo huu utajenga taifa lenye amani, upendo, na usalama thabiti kutokana na wananchi kuona wanathaminiwa na kusikilizwa katika kila hatua ya maendeleo ya nchi yao.
Wakitoa maoni mbalimbali, Katibu Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Bi. Fransisca Mboya, ameishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wadau katika mchakato wa kuandaa mwongozo huo, akisema umeandaliwa vizuri na umezingatia ushirikishwaji wa makundi katika ngazi mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Bw. Salehe Abdallah, amesema mwongozo huo utasaidia kuimarisha ushirikishwaji katika uendeshaji wa Serikali na michakato ya kufanya maamuzi.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani, Dkt. Isaya Mgalagu, amesema kazi kubwa imefanyika katika kuandaa mwongozo huo, akieleza kuwa unagusa ngazi mbalimbali za jamii kuanzia ngazi ya kitaifa hadi ngazi ya chini.
Ameongeza kuwa ushirikishwaji huo utasaidia kujenga taifa lenye umoja, upendo na mshikamano, akisisitiza kuwa wananchi wanapokuwa na mshikamano, huwa sehemu muhimu ya kulinda amani na usalama wa nchi.




