TANGAZO

TANGAZO

HAKUNA HABARI YENYE THAMANI KULIKO MAISHA YA MWANDISHI




Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kujiandaa kuripoti majanga yanayoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za Vuli, huku wakitanguliza usalama wao, kutoa taarifa sahihi na kuwaelekeza wananchi hatua za kujikinga.



Wito huo umetolewa wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitabiri kuwa msimu wa mvua za Vuli wa Oktoba hadi Desemba 2026 utaathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño. Kwa mujibu wa TMA, mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.


Akizungumza jijini Dar es Salaam Septemba 21, 2026, Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Mgaya Kingoba, amesema wananchi hutegemea taarifa za Waandishi wa Habari kufanya maamuzi ya kujilinda wakati wa majanga hivyo, utekelezaji wa jukumu hilo haupaswi kuhatarisha maisha ya Mwandishi.


“Wakati wa majanga, Mwandishi wa Habari anatakiwa kutimiza majukumu yake huku akilinda usalama wake na kuchukua tahadhari zote muhimu. Hakuna taarifa muhimu kuliko uhai wako,” amesema Kingoba.


Amesema Waandishi wa Habari wanapaswa kuthibitisha taarifa kabla ya kuzitoa kwa umma, akieleza kuwa taarifa zisizo sahihi zinaweza kusababisha hofu na taharuki. Amewataka kufuatilia utabiri na tahadhari za hali ya hewa kutoka TMA, pamoja na kupata taarifa za uokoaji na hatua za kukabiliana na maafa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Menejimenti ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa na halmashauri.


Kwa mujibu wa mwelekeo wa msimu uliotolewa na TMA, mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba katika ukanda wa Ziwa Viktoria, kisha kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba na ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Novemba.


Kingoba amesema wajibu wa Mwandishi wa Habari hauishii kueleza madhara yaliyotokea kwani unahusisha pia kuwafahamisha wananchi tahadhari za kuchukua, maeneo salama, mahali pa kupata msaada na hatua zinazochukuliwa na mamlaka.


“Mwandishi hatakiwi kuishia kueleza tatizo pekee, bali anapaswa pia kutoa taarifa za suluhisho; kwa mfano, kuwaeleza wananchi nini kifanyike, wapi wahamie, wapi wapate msaada na hatua zinazochukuliwa na Serikali,” amesema.


TMA imeeleza kuwa unyevu mwingi kwenye udongo na mafuriko vinaweza kujitokeza katika msimu huo na kina cha maji katika mito na mabwawa kinaweza kuongezeka, huku uchafuzi wa maji ukiweza kusababisha magonjwa.


Kingoba, ambaye pia ni Kaimu Meneja wa Huduma za Kiswahili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), amevitaka vyombo vya habari kutumia lugha inayotoa mwongozo bila kuongeza taharuki akisema Waandishi wa Habari wanapaswa kutathmini hatari za maeneo wanayokwenda, kuvaa mavazi yanayofaa, kulinda vifaa vyao vya kazi dhidi ya maji na kuepuka maeneo yenye mafuriko makubwa au uwezekano wa maporomoko.


Aidha, amesema wakati wa kuchukua picha na kufanya mahojiano, Waandishi wa Habari wanapaswa kulinda faragha, heshima na utu wa watu walioathiriwa na majanga huku pia wakiangazia mahitaji ya watoto, wanawake na watu wenye uhitaji maalum ili sauti zao ziwafikie wanaohusika na utoaji wa msaada.


Kingoba amevitaka vyombo vya habari kuanza maandalizi mapema kwa kuwapatia Waandishi wa Habari vifaa vinavyofaa na maelekezo ya usalama, ili waweze kuihudumia jamii bila kuhatarisha maisha yao.