-STAMICO Yazidi Kufungua Fursa kwa Wanawake Sekta ya Madini
Serikali imewataka wanawake wanaojihusisha na shughuli za madini kutumia ipasavyo fursa za maeneo na leseni wanazopewa kwa kuanzisha na kuendeleza shughuli zenye tija, ikisisitiza kuwa lengo si kuwa na idadi kubwa ya leseni pekee, bali kuziona zikigeuka kuwa migodi inayozalisha, biashara zinazokua, ajira na kipato kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, wakati akizungumza katika Hafla ya Utoaji wa Tuzo za Malkia wa Madini 2026 iliyofanyika Septemba 25, 2026 katika Golden Social Hall, mjini Geita, ambako alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa madini, kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, biashara na uongezaji thamani hadi utoaji wa huduma migodini.
Dkt. Kiruswa alisema hatua ya kutenga maeneo na kutoa leseni kwa wanawake inalenga kuwainua kutoka kuwa washiriki wa kawaida hadi kuwa wamiliki wa shughuli za uchimbaji, wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji, aliongeza kuwa kwa Mkoa wa Geita pekee, wanawake 714 wamejiunga katika vikundi mbalimbali na kupatiwa leseni ndogo za uchimbaji madini.
Dkt. Kiruswa alisisitiza kuwa utoaji wa leseni pekee hautoshi, akisema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo wanawake na wachimbaji wadogo katika teknolojia, usimamizi wa biashara, usalama na afya migodini, utunzaji wa mazingira, uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko. Aliwataka wanawake waliopatiwa leseni kuhakikisha maeneo yao yanaendelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na matumizi ya teknolojia sahihi ili shughuli za uchimbaji ziwe salama na endelevu. Aidha, alisema kupitia programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) na mipango mingine, Serikali inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika umiliki na uendelezaji wa rasilimali madini.
Dkt. Kiruswa alisema Serikali itaendelea kuhakikisha wanawake wanapata nafasi stahiki katika sekta hiyo, kwa lengo la kuwaona wakitoka katika nafasi ya washiriki na kuwa wamiliki wa migodi, wazalishaji wakubwa, wawekezaji, wafanyabiashara na watoa huduma wenye ushindani ndani na nje ya Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, alisema STAMICO itaendelea kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini kwa kuwapatia maarifa, teknolojia na msaada unaohitajika ili kuongeza tija na kukuza shughuli zao. Alisema STAMICO, kama mlezi wa wachimbaji wadogo, itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha wanawake wanapata mazingira bora ya kuendeleza shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kunufaika zaidi na fursa zinazopatikana katika mnyororo wa thamani wa madini.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Semeni Malale, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini pamoja na STAMICO kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuwawezesha wanawake kumiliki na kuendesha shughuli za madini. Alisema juhudi hizo zimeendelea kufungua fursa na kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali, STAMICO na TAWOMA ili wanawake wengi zaidi waweze kunufaika na fursa za maeneo ya uchimbaji, teknolojia, mitaji na masoko.
Katika usiku huo, Asha Msangi alitangazwa kuwa mshindi wa jumla na kutawazwa kuwa Malkia wa Madini 2026.



