Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) linaendesha zoezi la kufanya mapitio ya rasimu ya kanuni za majenzi (Building Codes) na maoni yaliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu kanuni hizo.
Zoezi hili la wiki mbili linaongozwa na timu ya wahandisi chini ya usimamizi wa Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Mhandisi Matiko Mturi (PhD).
Kanuni hizo zinatarajiwa kuwa muongozo wa kitaifa wa kusimamia usalama wa majengo, usalama wa watumiaji, na kuhakikisha majengo yanazingatia utunzaji bora wa mazingira, ndani na nje ya jengo.
Aidha, Mhandisi Mwakasenga ametoa wito kwa wadau wa sekta ya ujenzi kutumia kanuni hizo mara zitakapokamilika, akibainisha kuwa zitaleta manufaa makubwa kwa kupunguza athari zinazotokana na ujenzi usiozingatia viwango.
“Tunaomba wadau wote wa tasnia ya ujenzi kutumia kanuni hizi mara zitakapokamilika ili kupunguza au kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika ujenzi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Msanifu Majengo Arch. Mariahildergard Byarufu amesema kuwa kanuni hizi zitasaidia kuimarisha viwango vya ujenzi na kuhakikisha mazingira rafiki kwa watumiaji wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum. “Kupitia kanuni hizi, majengo yatakuwa na nafasi zinazokidhi viwango vinavyotakiwa, na kuwezesha kundi hili kutumia majengo bila kuhitaji msaada wowote,” amesema Arch. Byarufu.