Maafisa na Wakaguzi Mkoa wa Songwe wametakiwa kusimamia usalama na kuendelea kujipanga na uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2025.
Hayo yamesemwa Februari 24, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga wakati alipofanya kikao kazi na Maafisa na Wakaguzi katika ukumbi wa Polisi uliyopo Vwawa Wilaya ya Mbozi na kuwataka kuendelea kusimamia Askari katika himaya zao ili kutimiza jukumu mama la Jeshi la Polisi kwa kufuata sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili jamii iendelee kuwa salama.
"Endeleeni kutekeleza jukumu la kusimamia usalama wa raia na mali zao ikiwa ni pamoja na kujipanga na uchaguzi Mkuu, 2025 ili ufanyike kwa amani na usalama bila kujali itikadi ya chama chochote cha Siasa" alisema Kamanda Senga.
Kwa upande wao, Maafisa wamemshukuru Kamanda Senga na wameeleza kuwa wamejipanga vyema kwa kuweka mikakati endelevu ya kuimarisha usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu ili uchaguzi ufanyike kwa utulivu na amani.



