Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo hakina hoja ya msingi kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa malalamiko ya kutaka mabadiliko wanayoyazungumza yameshafanyika.
Amesema CHADEMA inadai haitashiriki uchaguzi hadi yafanyike mabadiliko ya kisheria yakiwemo ya uchaguzi, hata hivyo mabadiliko hayo yameshafanyika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Stendi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, Wasira alisema sheria zilizofanyiwa mabadiliko ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na madiwani.
Alisema nyingine ni Sheria ya Tume ya Uchaguzi pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa vinavyosimamiwa na msajili wa vyama vya siasa na kuongeza mambo hayo ndiyo waliyokuwa wakiyalalamikia.
“Moja wanasema wao hawataki uchaguzi wanasema tume ile inateuliwa na Rais moja kwa moja kwa hiyo sio huru, tukasema hamna tabu, wabunge wakaunda kwamba tuweke kamati maalumu ili mtu anayetaka ukamishna wa tume ya uchaguzi aombe na ipo hiyo inaongozwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar na watu kutoka Tume ya Haki za Binafamu na Utawala Bora.
“Kwa hiyo ukifika wakati atakayetaka ukamishna anaomba na huyo anayeomba anatazamwa kwa vigezo vilivyowekwa kulingana na kazi anayoomba, hiyo kamati ipo na maana yake ni kwamba mamlaka ya Rais yamepunguzwa…zamani alikuwa anaweza kuteua sasa hawezi, mpaka kamati ya usaili halafu imuambie Rais umehitaji watu watano tunakupa wanane chagua watano.”
Pia, Wasira alisema awali wapinzani walikuwa wakiwalalamikia wakurugenzi watendaji wa halmashauri kwa madai wanaiba kura hivyo hawataki wasimamie uchaguzi na walienda hadi Mahakama ya Afrika Mashariki kupinga wakurugenzi hao, sasa sheria mpya imewaondoa.
“Sasa tume itakuwa inateua watumishi wa umma waandamizi na watumishi waandamizi wa umma sio wote wanateuliwa na Rais hata ukienda vyuo vikuu utawakuta watumishi wa umma waandamizi, ni watu wasomi lakini hawateuliwi na Rais bali wanateuliwa na bodi za vyuo vyao na wanakuwepo kutokana na usomi wao.
“Wakiteuliwa watu wa namna hiyo na hasa watumishi wengine wa serikali waaminifu kusimamia uchaguzi na wakurugenzi waliokuwa wametamkwa kwenye ile sheria ya zamani wakaondolewa. Sasa hayo ndio mabadiliko makubwa ambayo yamefanywa, sasa imekuja hii hoja mpya mmeisikia na nyinyi ila inasemwa kwa kiingereza
“Inasema 'No Reform No election' eti wanataka mabadiliko zaidi ya yale yaliyofanyika sasa tunawauliza wabunge ndio wenye kazi ya kufanya mabadiliko ya kisheria na Bunge linavunjwa Juni 27 (2025) na wabunge wanarudi kwetu wanakuwa raia kama sisi, sasa uwalazimishe wafanye mabadiliko tena na presha ya ubunge iko juu,” alisema.
Aliongeza kuwa "eti wabunge wabaki bungeni kwa ajili ya 'reform' watakimbia hiyo 'reform' kwani hawapo wamemaliza muda wao kwa hiyo CHADEMA wanasema mambo ambayo hayawezekani. Unajua unaweza ukaeleza mambo hayatekelezeki hata wenye akili wakasema huyu anasema nini naye huyu."
“Sasa hilo wametoka wanasema wanataka reform ipi wakati reform tumefanya kumbe ile ni danganya toto kwa sababu wanaogopa uchaguzi wanakuja wakijua 'mtawapiga chini' walizoea kudanganya sasa udanganyifu mwisho, wamekuwa kama timu ya mpira inayoweka mpira kwapani.
“Siunajua timu ya mpira ikiweka mpira kwapani ujue wanaogopa, nazungumzia mpira wa siasa sio wa uwanjani. Sasa nawaambia haya ndio mambo, kwa hiyo badala ya kusema tunaogopa uchaguzi wanasema mpaka yafanyike mabadiliko, tutazuia uchaguzi,” alisema.
Makamu Mwenyekiti Wasira aliwaambia wananchi wa Kahama wajue CHADEMA hawana uwezo wa kuzuia uchaguzi na waeleze watazuia kwa kufanyaje maana Katiba inasema katika ibara ya 41 hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia uchaguzi wa Tanzania
Alifafanua kuwa, uchaguzi utaahirishwa kama kuna vita, na nchi haina vita sasa inaahairisha kwa sababu ipi au vita iko ndani ya vichwa vyao maana inawezekana wanatembea halafu ndani ya vichwa kuna vita inapiganwa.
“Uchaguzi unaanza kwa kujiandikisha, wakati wao wanaendelea na kelele za No Reform wenzao wanajiandikisha na Dar es Salaam maelfu ya watu wamejiandikisha mpaka siku zimeongezwa...achana na no reform achana na maneno yao, watu wanataka kupiga kura,” alisema.
== ==