TANGAZO

TANGAZO

UFARANSA YAKARIBISHWA KUWEKEZA KWENYE VIWANDA VYA KUTENGENEZA DAWA MUHIMU NCHINI TANZANIA


Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Ufaransa kuwekeza nchini Tanzania katika Sekta ya viwanda vya kuzalisha dawa za binadamu ili kukabiliana na upungufu wa dawa muhimu za binadamu hali inayosababishwa na mabadiliko sera za nchi mbalimbali duniani.

Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo jijini Paris nchini Ufaransa, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Bw. Bertrand Walckenaer.

Alisema Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inajipanga kutekeleza miradi ya ujenzi wa viwanda vitakavyozalisha dawa muhimu zikiwemo za malaria, kifua kikuu na dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) ili kulinda maisha ya watu.

Dkt. Nchemba alikuwa akijibu hoja ya Kiongozi huyo wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bw. Walckenaer, aliyetaka kufahamu mipango ya Serikali ya kukabiliana na mabadiliko ya Sera za Serikali ya Marekani ambayo imesitisha utoaji misaada kwenye sekta mbalimbali ikwemo ya Afya.

Aliishauri AFD kuiunga mkono Tanzania katika kutekeleza azma ya kujenga miundombinu ya viwanda vya uzalishaji wa bidhaa hizo ili kunusuru maisha ya mamia ya wananchi waliokuwa wakitegemea misaada ya dawa kutoka nje ya nchi na kwamba wawekezaji watanufaika na soko kubwa la bidhaa na huduma katika eneo lote la Maziwa Makuu na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

“Tunaikaribisha AFD kushirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na Sekta binafsi katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ili nchi iweze kujitegemea katika eneo muhimu la Afya”, alieleza Dkt. Nchemba.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Ufaransa imekuwa ikiisaidia Tanzania katika agenda za maendeleo kuanzia mwaka 1980, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam, maendeleo ya sekta ya nishati, maji na kilimo, miradi ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bw. Bertrand Walckenaer, alisema kuwa suala la nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuwa na viwanda vyake vya kuzalisha dawa ni muhimu kwa ajili ya mustakabali wa maisha ya wananchi wake.


Alibainisha kuwa hatua ya Marekani ya kufuta misaafa ya sekta ya afya na misaada ya kibinadamu zilizokuwa zikisaidia mataifa mbalimbali duniani kupitia Shirika lake la Misaada (USAID), zinasababisha kuwe na ulazima wa nchi zinazoendelea zilizokuwa zinanufaika na misaada hiyo kutafuta namna ya kukabiliana na hali hiyo.

Aliahidi kuishawishi sekta binafsi kutoka Ufaransa kuwekeza nchini Tanzania katika sekta ya afya kwa kujenga viwanda vya kutengeneza dawa ili kutimiza lengo na matarajio ya nchi katika kuwahudumia wananchi.

Alisifu mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania, pamoja na usimamizi mzuri wa uchumi wa nchi na mazingira mazuri ya uwekezaji unaopaswa kupigiwa mfano na mataifa mengine ya Afrika.

Bw. Bw. Bertrand Walckenaer, alisema Shirika la Maendeleo la Ufaransa limewekeza kiasi cha Euro bilioni 1.3 kwa miradi mbalimbali nchini Tanzania kutokana na utulivu wa sera na uchumi wake na kwamba wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya nchi hizo mbili. 

Fedha hizi zimeelekezwa kwenye miradi ya sekta za; Maji, Nishati, Miundombinu ya Usafirishaji, Kilimo na Maliasili na Utalii.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com