TANGAZO

TANGAZO

BoT YAKUTANA NA WADAU KUJADILI KANUNI ZA MATUMIZI YA FEDHA ZA KIGENI ZA MWAKA 2025

 


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekutana na wadau kutoka Chama cha Shule za Kimataifa Tanzania (TISA), Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT), Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya ARK kwa ajili ya majadiliano kuhusu Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025.

Vikao hivyo, ambavyo vimefanyika katika ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam, vimewaleta pamoja wadau hao kwa lengo la kujadili kwa kina Kanuni hizo ambazo zilichapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 198 la tarehe 28 Machi 2025.

Kwa mujibu wa Kanuni hizo, bidhaa na huduma zote zinazotolewa ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinapaswa kutozwa bei na kulipiwa kwa Shilingi ya Tanzania. Hivyo basi, ni kosa la kisheria kunukuu, kutangaza au kubainisha bei kwa kutumia fedha za kigeni; kulazimisha, kuwezesha au kupokea malipo kwa fedha za kigeni; au kukataa malipo yanayofanywa kwa Shilingi ya Tanzania.

Kanuni hizo pia zimeeleza aina ya miamala inayoruhusiwa kufanyika kwa fedha za kigeni, pamoja na kuweka ukomo wa muda kwa mikataba inayotekelezwa kwa fedha hizo. Aidha, kuanzia tarehe 28 Machi 2025, imekatazwa kuingia au kuhuisha mikataba mipya inayotaka malipo kufanyike kwa fedha za kigeni.

Kwa upande wa wageni kutoka nje ya nchi, wakiwemo watalii, watatakiwa kubadilisha fedha za kigeni kupitia benki za biashara au maduka ya kubadilisha fedha yaliyoidhinishwa. Pia wanaweza kuendelea kufanya malipo kwa kutumia kadi za kielektroniki au njia nyingine za kidijitali zilizozoeleka.

Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha utekelezaji wa Kanuni hizi unafanyika kwa ufanisi, kwa lengo la kuimarisha matumizi ya Shilingi ya Tanzania na kulinda utulivu wa soko la fedha nchini.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com