TANGAZO

TANGAZO

BoT YAONDOA TAHARUKI YA NOTI BANDIA CHAMWINO


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeondoa taharuki miongoni mwa wananchi wa Kijiji cha Igunguli, Kata ya Loje, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kufanya ukaguzi wa noti zilizodhaniwa kuwa bandia na kubaini kuwa fedha hizo ni halali.


Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia uvumi uliosambaa kuhusu uwepo wa noti bandia za shilingi 10,000, ambao ulisababisha hofu na wasiwasi kwa wananchi.


Katika jitihada za kurejesha utulivu kijijini hapo, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Bi. Janeth Mayanja, aliwataka wananchi kuzingatia sheria za nchi na kuepuka kuwa chanzo cha taharuki katika jamii. Alitoa wito huo tarehe 20 Mei 2025 alipowasili kijijini Igunguli kufuatilia hali hiyo iliyosababishwa na madai ya kuwepo kwa noti bandia.

Taharuki kuhusu uhalali wa noti za shilingi 10,000 ilizuka baada ya baadhi ya watu kuhoji tofauti za saini za Mawaziri wa Fedha wa vipindi tofauti. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kushukiwa kuwa na noti bandia, ambapo fedha zao zilichukuliwa na nyingine kuchanwa.

Timu ya wataalamu kutoka Tawi la Benki Kuu ya Tanzania, Dodoma, iliongozwa na Meneja wa Huduma za Kibenki na Sarafu, Bw. Nolasco Maluli, pamoja na Afisa Mwandamizi Bw. Atufigwege Mwakabalula na Afisa Uhusiano Mkuu Mwandamizi Bw. Lwaga Mwambande. Wataalamu hao walikagua noti sita zilizokuwa zikishikiliwa kwa tuhuma za kuwa bandia na kubaini kuwa zote ni halali kabisa.

Bw. Maluli alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu alama za usalama zilizopo kwenye noti halali, ambazo zinaweza kutambulika kwa kutumia macho, kupapasa kwa vidole na kutumia mwanga wa rangi ya zambarau. Alieleza kuwa tofauti ya saini za Mawaziri wa Fedha si kigezo cha kubaini uhalali wa noti, kwani saini hubadilika kadri ya mabadiliko ya uongozi.

Aidha, wananchi walihimizwa kutumia njia salama za kufanya miamala kama vile kutumia akaunti za benki na huduma za fedha kupitia simu badala ya kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha taslimu nyumbani, ili kuepuka hasara na taharuki zisizo za lazima.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com