TANGAZO

TANGAZO

DKT. KIRUSWA ATOA USHAURI UTATUZI MGOGORO ULIODUMU MIAKA 9


-Aunda timu ya maridhiano ya wajumbe 17

-Asisitiza maridhiano ya kweli ili kumaliza mgogoro baina ya wamiliki wa shamba na wamiliki wa leseni ya madini.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ametoa ushauri wa kufanya maridhiano ya kweli baina ya wamiliki wa mashamba na wamiliki wa leseni ya madini katika machimbo ya dhahabu yaliyopo katika eneo la Nyakafuru Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.


Dkt.Kiruswa ametoa ushauri huo leo tarehe 6 Juni, 2025 katika kikao maalumu kilichowakutanisha pande zote mbili zenye mgogoro na kuwashauri wafanye maridhiano ya kweli yatakayoleta tija kwa pande zote mbili kwa kuangali haki zilizopo kwa kila upande ambazo ni wamiliki wa mashamba na wamiliki wa leseni.



Katika kuhakikisha maridhiano hayo yanafanikiwa, Dkt.Kiruswa ameunda timu ya wajumbe kumi na saba watakaoshiriki katika mchakato wote wa kutafuta maridhiano kuanzia ngazi ya kijiji mpaka Mkoa.


Akielezea kuhusu majukumu ya timu hiyo, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, lengo la kuunda timu itakayosimamia maridhiano ni kuhakikisha haki zinapatikana kwa pande zote mbili hususan katika haki ardhi na haki madini, kufanya tathimini ya gharama husika na kufanya malipo kwa usawa na kuandaa mkataba maalum wa maridhiano utakaosainiwa na kuwasilishwa Wizara ya Madini.


Awali, akielezea kuhusu historia ya mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohamed amesema kuwa , mgogoro umekuwa wa muda mrefu ambapo mpaka sasa una miaka tisa bila kupata suluhu kwa pande zote, ambapo unapelekea wilaya ya Mbogwe kukosa mapato yanayotokana na uzalishaji wa dhahabu hivyo amewataka wahusika kutumia fursa iliyotolewa na Dkt. Kiruswa kuhakikisha mgogoro unamalizika kwa wakati.


Pamoja na mambo mengine, Sakina amempongeza Dkt.Kiruswa kwa juhudi mbalimbali anazofanya kuhakikisha mgogoro huo unakwisha kwa kutenda haki kwa pande zote mbili.


Akielezea kuhusu hali ya mgogoro Afisa Madini Mkazi wilaya ya Mbogwe, Mhandisi Jeremiah Hango ameeleza kuwa, mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu Ofisi ya Madini Mbogwe imefanya juhudi mbalimbali za kutatua mgogoro kuanzia ngazi ya kijiji mpaka wilaya lakini mpaka sasa muafaka bado haujapatikana.


Kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123, kifungu cha 95 na 96, kinasema mwenye shamba ana miliki sehemu ya juu ya ardhi , huku mwenye leseni anamiliki madini yaliyopo chini ya ardhi katika eneo husika la leseni.


Lakini utaratibu unamtaka mmiliki wa leseni kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji atatakiwa kuingia mkataba na mwenye ardhi.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com