TANGAZO

TANGAZO

SERIKALI KUJENGA UKUMBI MKUBWA WA KIMATAIFA WA MIKUTANO ARUSHA

 


Katika juhudi za kuimarisha Utalii wa Mikutano na Matukio (MICE) nchini, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza mchakato wa ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (Convention Centre) katika Mkoa wa Arusha, ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua washiriki zaidi ya 6,000 kwa wakati mmoja.


Taarifa hiyo imetolewa leo, Juni 6, 2025, na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, katika ufunguzi wa Maonyesho ya Karibu-Kilifair 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Magereza, Kisongo, jijini Arusha.


Mhe. Kitandula amesema kuwa kwa sasa Utalii wa Mikutano na Matukio unaendelea kukua kwa kasi, hasa katika Mkoa wa Arusha, na hivyo Serikali imeona umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ili kuboresha zaidi mazingira ya kuvutia mikutano na matukio ya kimataifa.


"Serikali imeshatangaza zabuni ya ujenzi wa Ukumbi huu mkubwa wa Kimataifa, ambao unatekelezwa chini ya usimamizi wa Taasisi ya AICC," amesema Mhe. Kitandula.

Ameongeza kuwa mradi huo pia utajumuisha hoteli za kisasa zenye uwezo wa kuwahudumia Marais watano kwa wakati mmoja, pamoja na kuwepo kwa huduma zote muhimu za kimataifa, ili kuhakikisha mazingira bora na ya kuvutia kwa washiriki wa mikutano na maonesho kutoka ndani na nje ya nchi.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com