UTANGULIZI Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizaliwa tarehe 27 Januari 1960 visiwani Zanzibar, ambako alikulia katika mazingira yaliyomjengea misingi ya uadilifu, bidii na huduma kwa jamii. Akiwa msichana mdogo, alianza safari ya elimu katika shule za msingi na sekondari za Zanzibar kabla ya kuendelea na masomo ya juu ya utumishi wa umma.
Katika kujiendeleza na ngazi ya elimu ya juu, Rais Samia alijiunga na IDM Mzumbe, ambako alihitimu Diploma ya Utawala wa Umma, kisha akapanua upeo wake wa kitaaluma kwa kusomea Uchumi katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza (UK).
Alihitimu Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kupitia ushirikiano wa Open University of Tanzania na Southern New Hampshire University ya Marekani.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dunia na taasisi mbalimbali zimetambua mchango wake katika uongozi na siasa umetambuliwa kimataifa kwa kutunukiwa shahada za heshima (Honoris causa) na taasisi mbalimbali za elimu ya juu, ambavyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Ankara (Türkiye), Jawaharlal Nehru University (India) na Korea Aerospace University (Korea Kusini). SAFARI YA KISIASA Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan alianza rasmi safari yake ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 1987.
Katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alishika nafasi mbalimbali ikiwemo Naibu Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadaye Waziri kamili. Mwaka 2010, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Makunduchi na aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira, mwaka 2014, aliteuliwa kuwa makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba.
Mwaka 2015 alivunja rekodi alipoteuliwa kuwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa CCM Dkt ,hayati John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu wa 2015 na kufanikiwa kushinda uchaguzi na hatimaye alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.
Baada ya kifo cha Rais Dkt. John Magufuli, tarehe 19 Machi 2021, Samia aliapishwa kushika nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimataifa na kikanda Rais Samia amefanikiwa kuhudumu kama Mwenyekiti wa Troika ya Kamati ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama (2024/25). Katika uchaguzi wa mwaka huu Dkt. Samia Suluhu Hassan amevunja rekodi ya kuwa mgombea wa Urais mwanamke wa kwanza ndani ya CCM tangu CCM ianzishwe mwaka 1977 (awali TANU, 1954).
FALSAFA YA UONGOZI NA MAGEUZI YA KISIASA Tangu aingie madarakani mwaka 2021 Dkt. Samia Suluhu Hassan amebuni
falsafa ya “4R” yaani Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na kujenga Upya.
Kupitia falsafa hii, amefanikiwa kuliunganisha Taifa kisiasa na kijamii kwa kuimarisha maridhiano na umoja wa kitaifa. Ambapo katika hatua za haraka kama jitihada za kuunganisha Taifa na utawala bora aliondoa marufuku ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Sambamba na kuwachilia wafuasi wa vyama vya upinzani takriban 400 kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwemo viongozi waandamizi wa upinzani sambamba na kuwarudisha nchini waliokimbia nchi kutokana na mazingira yaliokuepo ya kisiasa. Katika nyanja ya uchumi, Rais Samia amewekeza katika diplomasia ya uchumi.
Kupitia filamu ya “The Royal Tour” mwaka 2022, alionesha mfano kwa kushiriki moja kwa moja katika kucheza filamu hii iliyosaidia kuvutia na hatimaye kuongeza idadi ya utalii nchini kutoka 922,000 mwaka 2021 hadi milioni 2.1 mwaka 2025 iliyosaidia kuongeza mapato ya utalii kutoka dola za marekani bilioni 3.1 mwaka 2021 hadi dola bilioni 3.9 mwaka 2025.
Sambamba na mafanikio haya amefanikiwa kuanzisha na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati kama vile Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, SGR, ujenzi na ukamilishaji wa madaraja makubwa kama vile Kigongo(Busisi), Wami na Tanzanite kutaja kwa uchache.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake vijiji vyote vimefikishiwa huduma ya nishati ya umeme.
Katika nyanja ya kimataifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitangaza na kuipata nchi yetu heshima na kulitambulisha taifa letu ambapo kwa uchache mwaka 2023, Tanzania ilipata heshima ya kualikwa (Guest Country) kwenye mkutano wa G20 uliofanyika India, mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ujulikanao kama Mission 300 uliofanyika Januari 27 na 28, Dar es salaam ukihusisha wakuu wa nchi zote 54 Afrika pia mwenyeji wa mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa (maarufu G-25 African Coffee Summit) uliofanyika kuanzia Februari 21-22, 2025.
Vilevile katika kipindi chake cha miaka minne amefanikiwa kualikwa katika mataifa makubwa kama vile Marekani, China, Umoja wa Ulaya na barani Asia.
Vilevile amefanikiwa kushawishi ziara rasmi ya viongozi wa mataifa mbalimbali kama vile ziara ya makamu wa Rais wa Marekeni Kamala Harris mwaka 2023.
