TANGAZO

TANGAZO

RAIS SAMIA AWASHUKURU WANANCHI WA UYUI - TABORA , AAHIDI KUTEKELEZA SEKTA SITA MUHIMU

 


Mgombea wa Urais kupitia CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwashukuru wananchi wa Uyui kwa mapokezi makubwa na kuwakumbusha ziara yake ya tarehe 17 Mei 2022 ambapo alifungua barabara ya kilomita 85 ya Nyahua–Chanya. 

Alisema wakati huo wananchi walimueleza changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya na elimu, na sasa serikali imewaletea watumishi wa afya 161 na walimu 412.

 Aidha, alikumbusha kuwa ndani ya siku 100 za uongozi wake serikali itaweza kuajiri watumishi 5,000 katika sekta ya afya na 7,000 katika sekta ya elimu, na baadhi yao watapelekwa Uyui. 

AFYA 

Mgombea wa Urais kupitia CCM Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema shilingi bilioni 8.2 zimetumika kuboresha hospitali ya wilaya, kujenga vituo vya afya vipya vitano, zahanati mpya 17 na kupeleka magari matatu ya wagonjwa. 

Mhe. Dkt. Samia amewaahidi wananchi wa Uyui kuwa endapo watamchagua yeye na wagombea wa CCM, itaendelea kusaidia kukamilisha vituo vya afya ambavyo wananchi wameanzisha, hususan katika maeneo ya Goweko na Usagari. 

ELIMU 

Kuhusu sekta elimu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema shule za sekondari zimeongezeka kutoka saba hadi 34 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, huku idadi ya wanafunzi ikipanda kutoka 12,000 hadi 17,500. 

Aliongeza kuwa shule za msingi zimeongezeka kutoka 158 hadi 182, na serikali imeendeleza sera ya elimu bila ada, kujenga madarasa ya chekechea na kuanzisha programu mpya za elimu ya awali.

Kukamilisha ujenzi wa chuo cha VETA na kuweka viwanda vidogovidogo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya vijana. 

KILIMO

Akizungumzia kilimo na mifugo, Dkt. Samia amesema serikali imejenga skimu za umwagiliaji katika maeneo ya Goweko na Ulianyama, na imeendelea kutoa ruzuku za mbolea na mbegu pamoja na dawa za chanjo kwa wafugaji. 

Amesema kuwa endapo itachaguliwa tena kuongoza na kuunda serikali katika uchaguzi mkuu wa Oktoba itaendelea kujenga majosho na mabwawa kwa ajili ya mifugo. 

Alizungumzia pia wakulima wa tumbaku wenye madai ya muda mrefu Dkt. Samia amewahidi kuwa serikali ipo kwenye mazungumzo na kampuni husika na wakulima watalipwa. 

Alisema serikali imeongeza makampuni ya kununua tumbaku ili kuleta ushindani. 

MAJI 

Kuhusu sekta ya maji, mgombea wa Urais Dkt. Samia amesema serikali yake imekamilisha miradi 15 ya maji ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma kufikia asilimia 67, Dkt. Samia amewaahidi wananchi wa Uyui kuwa iwapo watamchagua atajenga tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja kupitia mradi wa Ziwa Victoria katika kata ya Ilolangulu litakalohudumia pia kata za Kalola, Isila, Dono na Mabana. 

Aliongeza kuwa miradi mingine katika Kigwa, Kizengi na bwawa la Igombe ipo katika hatua nzuri na itakamilishwa. 

MIUNDOMBINU 

Kuhusu miundombinu, Mhe. Dkt. Samia amewajulisha wananchi kuwa usanifu wa Daraja la Mto Loya umekamilika, fedha zimetengwa na sasa serikali yake itakapopewa ridhaa na watanzania hasa wa Uyui itaendelea kuboresha barabara za vijiji ili ziweze kupitika wakati wote, ikiwemo barabara ya Ilolangulu–Isenga–Kasisi A na barabara ya Ndono–Mfuluma–Makazi.

 Aidha, alisema ombi la barabara ya Tabora–Kahama limepokelewa na serikali italifanyia kazi. 

UMEME 

Mgombea wa Urais kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaomba wananchi wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kukichagua chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili serikali yake iweze kufikisha umeme katika vitongoji 

vyote vilivyosalia kwenye wilaya ya Uyui katika kipindi cha mwaka 2025-2030, kwani kwa miaka mine ya uongozi wake 2021-2025 ameweza kufikisha umeme katika vijiji vyote na sasa kazi iliyobaki ni vitongoji. 

URAMBO- TABORA 

Mgombea wa Urais kupitia CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na mikutano ya kampeni katika mkoa wa Tabora ambapo amefanya mkutano mkubwa wa hadhara akiwa Urambo ambapo amewahakikishia wananchi wa Urambo kuwa chama cha Mapinduzi (CCM) kikipewa ridhaa na watanzania hasa wa jimbo la Urambo kitaendelea kutekeleza ahadi zake kwa vitendo. 

Dkt. Samia amesema chama kimetekeleza asilimia 90 ya ilani ya uchaguzi wa 2020-2025 na kipo katika hatua za kukamilisha machache yaliosalia.

KILIMO/ ZAO LA TUMBAKU 

Akizungumza kuhusu zao la tumbaku ambalo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Urambo, Mhe. Dkt. Samia amesema uzalishaji umeongezeka kutoka tani 11,208 mwaka 2021/2022 hadi tani 20,492 mwaka 2025. 

Aliongeza kuwa thamani ya mauzo imepanda kutoka dola milioni 11 mwaka 2021/2022 hadi dola milioni 50 mwaka 2024/2025, huku bei ya tumbaku pia ikiongezeka kutoka dola moja kwa kilo hadi dola 2.5 kwa kilo. 

Alisema awali tumbaku ilinunuliwa kwa kuchaguliwa lakini sasa serikali imehakikisha kuwa makampuni yananunua yote, na kiwanda cha kuongeza thamani kipo Morogoro kabla ya kusafirishwa nje ya nchi. 

Katia hatua nyingine Mhe. Rais Samia ambaye pia ni mgombea wa Urais kupitia CCM aliwaasa wakulima kupunguza ukataji miti na kutumia teknolojia mpya ya kukausha tumbaku ili kulinda mazingira, kuongeza mvua na kuhifadhi vyanzo vya maji. Pia alieleza kuwa serikali yake imeimarisha sekta ya kilimo kwa kujenga skimu mbili za umwagiliaji katika maeneo ya Uyogo na Izimbili, na kuanzisha soko la mazao. 

ELIMU 

Kuhusu elimu, Mhe. Dkt. Samia ameomba wananchi wa Urambo kumchagua yeye sambamba na wagombea wengine wa CCM ili kufanikisha ujenzi wa shule 12 mpya za msingi na sekondari sambamba na kuendeleza na kuboresha miundombinu ya Elimu katika jimbo la Urambo. 

MIUNDOMBINU 

Akizungumzia miundombinu ya barabara, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni mgombea wa Urais wa kwanza mwanamke ndani CCM, amewaambia wananchi wa Urambo kuwa serikali yake imejenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Emirates–Mnyonge–Usoke, Urambo–Izimbili– Mabama, Tebela–Uwima, Usoke–Kalembela na Kindwa. 

Amewaomba wananchi wa Urambo kumchagua ili aendelee kujenga barabara za Urambo kwa kiwango cha lami katika maeneo yote muhimu. 

Aidha, Dkt. Samia amewaahidi wananchi wa Urambo serikali yake ikipata ridhaa itajenga soko jipya katika mtaa wa St. Vicent na kuendeleza ujenzi wa vibanda vya biashara katika stendi kuu ya mabasi. 

Aliongeza kuwa huduma za afya, umeme na maji bado zitaendelea kupewa kipaumbele na serikali itaendelea kuzitekeleza kulingana na mahitaji ya wananchi. 



Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com