TANGAZO

TANGAZO

POLISI WAKEMEA MATUMIZI MABAYA YA MTANDAO KULETA HOFU



Na.  Mwandishi wetu

Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kali kwa kundi la watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kusambaza chuki, taharuki, na propaganda za kuvuruga amani, likisisitiza kuwa vitendo hivyo ni uhalifu wa wazi na si uhuru wa maoni.

Akizungumza kwa msisitizo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda David Misime, alitoa kauli thabiti akisema, "Amani ya nchi yetu ni tunu isiyopaswa kuwekwa rehani kwa jazba au tamaa za wachache wenye nia ovu."

Kamanda Misime alieleza kuwa Jeshi la Polisi limebaini ongezeko la tabia za kiuhalifu zinazofanyika kupitia majukwaa ya mtandaoni, akizitaja kama:Kuhamasisha vurugu na maandamano yasiyo halali,Kueneza upotoshaji wa taarifa na chuki miongoni mwa wananchi,Kuvunja misingi ya sheria, maadili, na utamaduni wa Kitanzania.

"Tunawakumbusha Watanzania wote kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Ujumbe wowote wa chuki, uchochezi, au ule unaolenga kuvuruga amani ya nchi yetu utashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za nchi. Huu si uhuru wa maoni, huu ni uhalifu," alikariri Kamanda Misime.

Akitoa onyo la moja kwa moja kwa wale wanaojihusisha na uhalifu huo, Kamanda Misime alisisitiza kuwa operesheni ya kuwakamata inaendelea.

"Kwa wale wanaoendelea kutumia mitandao kueneza vurugu na uongo, wajue wazi kuwa Sheria Ipo Macho, na muda wao ni mdogo. Jeshi la Polisi litaendelea kuhakikisha kuwa wote wanaojihusisha na uhalifu huu wanachukuliwa hatua za kisheria bila upendeleo," alisema.

Mwisho, msemaji huyo wa polisi alitoa wito kwa wananchi wote wenye mapenzi mema na taifa lao kuwa walinzi wa amani.


"Tunaiita jamii iwe sehemu ya suluhisho. Tuikatae jamii ya ujumbe wa chuki. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kulinda utulivu wa nchi yetu na kuilinda familia yake dhidi ya machafuko yanayochochewa na watu wachache. Watanzania tuilinde amani yetu, tuheshimu sheria, na tukatae upotoshaji wa mitandaoni," alisema Kamanda Misime.


@@@@@@@@@@@@@@


MAZOEZI NI KINGA YA TAIFA, SIO VITISHO


Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini vimeendelea kufanya mazoezi ya pamoja, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni utaratibu wa kawaida wa kijeshi unaolenga kuimarisha utayari na weledi na wala si mbinu ya kuwatisha wananchi.


Kauli hii inatolewa kufuatia kuwepo kwa upotoshaji wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii, unaodai kuwa mazoezi hayo yanatumika kama vitisho au mbinu za kukandamiza.


Vyombo hivyo vimekiri kuwa kuna propaganda hizo zisizo na msingi zinazoenezwa mtandaoni zinafanywa kwa lengo la kuchochea hofu na kuhalalisha maandamano haramu.


Wito umetolewa kwa wananchi wote kupuuza uzushi wa mitandaoni na kutambua kuwa mazoezi haya ni ngao ya taifa, si tishio kwa wananchi.


"Huu ndio uthibitisho kwamba Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani, salama, na thabiti. Mazoezi haya ni kinga yetu kama taifa," ilihitimisha taarifa hiyo.


Vikosi vya ulinzi vimekumbusha umma kuwa mazoezi ndiyo shughuli yao ya msingi, na hakuna sababu yoyote kwa wananchi kuwa na hofu. Lengo la msingi la mazoezi ya pamoja ni kupima uwezo wa vikosi vyote wakati wa kushughulikia mambo mbalimbali yanayohusu taifa, ikiwamo:Ulinzi wa mipaka na amani ya taifa;Kukabiliana na maafa (mfano: tetemeko la ardhi, mafuriko au majanga mengine) na Kudumisha mshikamano wa kiutendaji kati ya vyombo vyote vya ulinzi.


"Mazoezi haya, yanayojumuisha matembezi ya pamoja, mafunzo ya viungo, na mazoezi ya kivita, yanaboresha afya za askari, yanaongeza weledi wa kazi, na kujenga mshikamano wa kikazi," ilisema taarifa iliyotolewa na vyombo hivyo.


Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimesisitiza kuwa mazoezi mengi hufanyika hadharani katika barabara na maeneo ya wazi ili kuonyesha uwazi na kuhakikisha wananchi wanatambua utayari wa vyombo vyao vya ulinzi.


"Ukweli unabaki palepale: wananchi wengi wameona kwa macho yao kuwa mazoezi haya ni kielelezo cha utayari wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com