Kabila la Wahadzabe ni moja ya makabila yaliyopo eneo la hifadhi ya Ngorongoro, makabila mengine ni pamoja na wamasai na wadatoga ambapo kwa pamoja yanaguswa na mradi wa Jiopaki ya Ngorongoro maarufu kama Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark ambayo kwa sasa imeasisi uanzishwaji wa makumbusho kubwa na ya kisasa iliyopo Wilayani Karatu inayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Makala haya inaangazia thamani ya mnyama nyani katika kuoa kwenye kabila la wahadzabe. Kwa mujibu wa wazee mbalimbali wa kabila hilo, katika maisha yao ya kila siku jamii hii huishi kama kundi moja linaloshirikiana bila utengano wa familia au ukoo tofauti na makabila mengine nchini ambayo hutambuana pia kwa kutumia ukoo.
Wahadzabe katika jiopaki ya Ngorongoro wanapatikana pembezoni mwa Ziwa Eyasi ambapo wameweka maskani yao na kuendeleza maisha yao ya jadi kwa kuwinda, kurina asali na kuchimba mizizi ambapo mfumo huo wa Maisha yasiyobadilika yamepambwa na kila aina ya silka, tabia na taratibu za utamaduni wa jadi.
Jambo usilolijua na la kusisimua ni kuwa kijana anapotaka kuoa katika kabila la Wahadzabe ni lazima awe shupavu na hodari wa kuwinda wanyama na kijana hutakiwa kuhakikisha kuwa ana uwezo wa kukabiliana na wanyama wakali wanaoishi porini na moja kati ya sifa za kuoa katika kabila hili ni kuhakikisha kuwa una uwezo wa kuua wanyama wakubwa.
Kijana aliyefikisha umri wa kuoa ili akabidhiwe mke ni lazima aue Madume mawili ya nyani, Pundamilia mmoja, Pofu mmoja na madebe mawili ya asali ambayo ndio yanakamilisha mahari, hivyo mshenga wa kihadzabe hutakiwa kupeleka ukweni na hapo ndipo unaweza kukubaliwa posa na kukabidhiwa mke.
Kichwa cha nyani siku ya harusi huliwa na baba mkwe kudhihirisha kuwa hiyo ni heshima ya baba mzaa chema ambapo hakuna mtu mwingine katika jamii hiyo atakayeruhusiwa kula kichwa hicho na hivyo kumfanya baba mkwe kujisikia kuwa kweli anaheshimika kwa kumuozesha binti yake kwenda familia nyingine.
Je wataka kujua zaidi? Naaam, Ulaji wa kichwa cha Nyani kwa baba mkwe siyo siku ya Harusi tu laa hasha, kijana hukabiliwa na mtihani wa kupeleka kichwa cha mnyama huyo kwa baba mkwe hata baada ya kuoa kwa maana nyingine kila ndani ya nyumba anapoliwa nyani kichwa chake lazima kipelekwe kwa baba mkwe.
Kwa kabila la wahadzabe nyani ndiyo mnyama mwenye thamani kuliko wanyama wote hii ni kutokana na utamu wa nyama yake ambapo jamii hiyo huamini kuwa nyama ya Nyani ni tamu kutokana na mnyama huyo kula matunda matamu ambayo binadamu pia anakula hivyo kuwa na nyama ambayo utamu wake hauelezeki labda mpaka uijaribu hivyo thamani yake inakuwa kubwa kulinganisha na Wanyama wengine ambao wanakula majani.
Kutokana na sababu hizo ndio zinaifanya jamii ya Wahadzabe kumtumia mnyama huyo na nyama yake katika matukio yote ya kijamii ikiwemo kupatikana kwa mtoto, harusi, misiba na matambiko mbalimbali ya kijamii.
Dhana na imani hii ni tofauti na jamii ya waswahili ambapo suala la ushenga huzingatia umri, hekima na kuaminika kwa mtu katika familia inayooa. Jamii ya wahadzabe mchakato wao wa kuoa huanzia kwa wahusika wenyewe kwa muktadha wa muoaji na muolewaji kukubaliana kuwa wana upendo wa kweli.
Kwa jamii hii, suala la Mshenga sio muhimu sana hata kama ana umri, hekima na busara zinazotakiwa isipokuwa kitu cha kwanza kinachotakiwa ili uweze kupata mke katika jamii ya wahadzabe ni uwezo usiokuwa na shaka katika kulenga mshale na kuua mnyama muhimu kama Nyani,kwa kufanya hivyo unadhihirisha kwamba wewe ni mwamba na unastahili kupata mwari wa kihadzabe.
Kwa jamii ya wahadzabe wanyama wakubwa wengine ambao wahadzabe huwapenda ni Kudu, Pofu na Twiga ambapo katika jamii hii kwa sasa kumekuwa na changamoto ya kuwapata wanyama hao tofauti na miaka ya nyuma kutokana na sheria na taratibu za uhifadhi wanyamapori.
Uwindaji sio tu chanzo cha chakula, bali ni uthibitisho wa ulinzi, ujasiri na uwezo wa kuongoza familia ambapo wazee huanza kuwachunguza vijana wanapofikia umri wa balehe na wakishajiridhisha kwamba kijana husika ni hodari kijana hupimwa kwa kupewa mshale wenye sumu kidogo ili aweze kwenda kuwinda.
Akiwa katika mawindo yake kijana atakapomuona mnyama mkubwa kama nyani, kumlenga na kumuua hurudi nyumbani na kutoa taarifa kwa wazee ambapo wazee hao sasa huenda kuangalia kama kweli kijana huyo amefanikiwa kuua mnyama huyo kutokana na vingezo vilivyowekwa.
Katika kabila la wahadzabe ndoa ni maridhiano baina ya watu wawili na hufanyika siku yoyote ile baada ya masharti kutimizwa na tofauti na harusi za kisasa wao hawana siku maalum iliyopangwa bali ni muda wowote na wakati wowote kijana muoaji anapofanikiwa kuua mnyama ingawa ikibidi hutakiwa kufanya tendo la ndoa kabla ya harusi kufanyika.
Tofauti na makabila mengine baada ya harusi kufanyika kijana hukabiliwa na mtihani mwingine, nao ni kulazimika kuishi kwa wiki moja ukweni, ukiwa ukweni wazazi wa binti huanza kukufuatilia kama kweli wewe una sifa za mwanaume ikiwa ni pamoja na uwezo wa kutunza nyumba na kuishi na familia.
Katika kipindi chote cha wiki moja wazazi wa binti humchungumza bwana harusi kwa karibu ili kuona tabia, heshima na uwezo wake wa kuishi na familia, hii ni hatua ya ukomavu na kukubalika na iwapo wazazi wameridhika na mwenendo wa mwanaume basi binti ndio hupelekwa ukweni na wazazi wake.
Katika kipindi chote ambapo kijana anakuwa ukweni ndio atakayekuwa na jukumu la kuwinda porini na kuleta chakula kwenye familia ili kuonyesha kuwa anastahili kumchukua binti wa kihadzabe na kwenda kuishi naye katika mji wake.
Aidha, kwa kuwa kipindi hicho cha wiki moja kijana atakuwa anakula vizuri nyama za porini hasa nyani basi wahadzabe huamini kwamba mpaka watakapomruhusu kurudi katika mji wake ndoa ya kijana huyo itakuwa imejibu na hapo ndipo mwanzo wa familia mpya kuanza.
Ukitaka kujua mengi zaidi kuhusu jamii hii Karibu makumbusho Urithi Geopark Museum.





