TANGAZO

TANGAZO

VIONGOZI WA DINI NA WADAU WAUNGANA KUSISITIZA AMANI NA UMOJA

 


Katikati ya hali ya sintofahamu inayochochewa na miito ya maandamano yasiyo na kikomo kutoka kwa baadhi ya wachochezi wa nje, Watanzania wameibuka na umoja wa dhati, wakisisitiza umuhimu wa amani, umoja na ushirikiano kama tunu za msingi za maendeleo ya nchi.


Wito huu umetiwa nguvu na tangazo la Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar Zubeir, kuhusu kuanza kwa mazungumzo ya viongozi wakuu wa taasisi za dini nchini kurudisha nchi katika taswira yake ya amani na kulinda maisha na mali za Watanzania.

Mufti Zubeir alithibitisha kwamba taasisi za dini, kupitia Tanzania Interfaith Partnership (TIP), zimeanza mazungumzo ya kina yakiongozwa na Katibu Mkuu wa BAKWATA.

"Makatibu wakuu wa TEC, CCT na Bakwata tayari wamekutana mara kadhaa na hatimaye sisi viongozi wakuu pia tulikutana," alifafanua Mufti, akiongeza kuwa lengo kuu ni "kuinusuru nchi yetu na kulinda maisha, mali iwe za umma au za watu binafsi, miundo mbinu na kuirejesha nchi yetu katika taswira yake."

Wito huu wa amani uliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Amon Mpanju, ambaye aliwataka viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii, wasanii, na viongozi wa vyama vya siasa kudumisha amani ya Tanzania.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Morogoro, Sheilla Lukuba, alielezea wasiwasi wake kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, akitaja kizazi cha sasa ni "kizazi cha utandawazi." Aliomba wazazi kutoacha pengo kubwa katika kuwaelekeza watoto wao, akisisitiza: "Tumeshaanza kuona madhara yake, tuendelee kuwasaidia watoto, kuwaongoza ili taifa letu lisitoke kwenye elimu ambayo wazazi wetu walitupa."

Mkazi wa Mzumbe na fundi ujenzi, Nuhu Ally, alitoa ushauri kwa vijana wenzake: "Ninawashauri vijana wenzangu kuitumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kujikwamua kiuchumi na si kuhamasishana mambo yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani."

Mufti Zubeir pia alitoa mwito mkali kwa wale wote wanaosukumwa na kuhamasisha fujo na uvunjifu wa amani, akiwataka waache mara moja kufanya hivyo kwani kunahatarisha maisha ya watu. Aliwaomba Watanzania wawe watulivu na walinda amani, huku akiwaonya juu ya upepo mbaya wa chuki za kidini.

Aliwataka wazazi kuwapa nasaha vijana wao wasikubali kutumika kama mtaji wa watu wachache wasioitakia mema nchi. Zaidi ya hayo, aliwataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi kutumia fursa zao kuisaidia nchi badala ya kukubali kutumika kuiingamiza, akisisitiza msemo kwamba "kuipenda nchi ni ukamilifu wa imani."
Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com