Wakati kelele za wapotosha zikijaribu kuzima mafanikio ya Taifa kupitia mitandao ya kijamii, Jumuiya ya Kimataifa imetoa tamko zito la kumtambua na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kama kiongozi shupavu aliyefanikiwa kuvuka mawimbi ya machafuko na kuimarisha amani nchini Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amebainisha kuwa viongozi wa mataifa yenye ushawishi mkubwa na Umoja wa Mataifa (UN) wamevutiwa na namna Rais Samia alivyoweza kudhibiti hali ya usalama kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Katika mikutano ya faragha nchini Ethiopia, viongozi kama Rais wa Angola, João Lourenço, na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, wamempongeza Rais Samia kwa ukomavu wa kisiasa na ujasiri wa kulinda utulivu wa Tanzania.
Balozi Kombo ameweka wazi kuwa viongozi wa dunia wamebaini siri iliyojificha: kwamba maandamano na vurugu zilizojaribu kuchochewa si matakwa ya wananchi, bali ni "wimbi la kidunia" la matumizi mabaya ya teknolojia yanayolenga kuvuruga mataifa imara ili kugombea rasilimali. Hatua ya Rais Samia kusimama kidete na kuhakikisha Watanzania wanaendelea na shughuli zao kwa amani, imetajwa kama mfano bora wa uongozi barani Afrika.
Dunia haijamsaidia Rais Samia kwa bahati mbaya. Mataifa ya Afrika yanakumbuka fadhila za Tanzania katika ulinzi wa amani na msaada wa chakula wakati wa majanga.
"Kumpa moyo Rais Samia ni kuwapa moyo wanawake wote wa Afrika wanaofanya kazi kwa bidii," alisema mdau mmoja wa diplomasia, akijibu baadhi ya maoni ya kubeza yanayotolewa na watu wasioitakia mema nchi yetu.
Wakati baadhi ya wachache mitandaoni wakidai "matango pori," ukweli unabaki kuwa Rais Samia ameshinda mioyo ya Watanzania na heshima ya dunia. Kivuli cha chuki hakikimbiwi, bali kinapotea jua la ukweli linapochomoza na leo jua la uongozi wa Samia limechomoza kote Afrika na duniani.
Tanzania ya sasa ni nchi ya amani, utulivu, na maendeleo. Wanaojificha nyuma ya vibodi (keyboards) kutaka vurugu hawatafanikiwa, kwani Watanzania wamechagua kiongozi anayeunganisha badala ya kugawanya.
