TANGAZO

TANGAZO

SERIKALI YAWEKA UWAJIBAKAJI SEKTA YA ARDHI




Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameutumia uzinduzi wa “Samia Ardhi Kliniki” jijini Dar es Salaam kutangaza msimamo mkali wa Wizara dhidi ya vitendo vya uzembe na ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi.



Katika hafla hiyo, Waziri Akwilapo amesema Wizara imeamua “kujivua gamba” na kuanza ukurasa mpya wa uwajibikaji, akisisitiza kuwa kauli za watumishi kudai mafaili kupotea au kutoonekana hazitavumiliwa tena.



“Hakuna kitu kama faili kupotea. Ofisi zetu zina mifumo thabiti, na mafaili hayana miguu ya kutoroka. Kauli hizi nimezipiga marufuku rasmi,” alisisitiza.


Waziri huyo alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi yanayolenga kurejesha imani ya wananchi kwa sekta ya ardhi, ambayo imekuwa ikikabiliwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu urasimu na usumbufu usio wa lazima.

Alisema Wizara haitasita kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa watumishi watakaobainika kukwamisha huduma kwa maslahi binafsi, akisisitiza kuwa ardhi ni rasilimali ya Taifa na watumishi ni wasimamizi tu, si wamiliki.

Uzinduzi wa “Samia Ardhi Kliniki” umefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Kliniki hiyo itafanyika nchi nzima kuanzia Machi 2 hadi 7, 2026, ikitoa huduma za msaada wa kisheria, utoaji wa hatimiliki na elimu ya taratibu za umilikishwaji wa ardhi.


Mbali na kuhimiza wanawake kujitokeza kunufaika na huduma hizo, Waziri Akwilapo aliwataka wanaume na viongozi wa kaya kuachana na mila potofu zinazowanyima wanawake haki ya kumiliki ardhi.


Kwa mujibu wa Waziri, idadi ya wanawake wenye hatimiliki imeongezeka hadi wastani wa asilimia 28 kutoka chini ya asilimia 10 miaka ya nyuma, hatua aliyoitaja kuwa ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita.


Kauli mbiu ya zoezi hilo ni: “Mwanamke; Haki Yako, Miliki Ardhi Sasa,” ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha usawa wa kijinsia na kuimarisha uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.


Awali Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw Edward Mpogolo akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Bw. Albert Chalamila mbali na kuipongeza Wizara ya Ardhi kwa kuanzisha Samia Ardhi Kliniki, amesema kuna baadhi ya changamoto zilizoanza kujitokeza kwa wale wanaopata hati miliki za ardhi kufunga barabara zinazotumika kwa jamii.


Ameomba utaratibu wa fomu za kuthibitishwa na majirani katika maeneo yaliyorasimishwa kuzingatiwa kwa kupitishwa katika ngazi husika na kusimamiwa ili kuepuka changamoto kama hizo.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera amesema, huduma kubwa zinazotolewa kupitia Samia Ardhi Kliniki ni elimu hususan ya haki za umiliki kwa wanawake, ushauri wa mambo mbalimbali ya sekta ya ardhi, utoaji hati kwa waliokamilisha taratibu pamoja na huduma nyingine.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com