TANGAZO

TANGAZO

AMANI NDIYO NGUZO YA UHURU NA MAENDELEO YA WATANZANIA


Na. Mwandishi wetu

Balozi wa amani nchini, Victor Victor ambaye anafahamika zaidi na Watanzania wengi kwa majina ya Nanga au Babu Kaju, amewataka wananchi kuendelea kuilinda na kuitunza amani iliyopo kwani ndiyo msingi wa kila kitu katika taifa. Akizungumzia umuhimu wa utulivu huo, Nanga amebainisha kuwa amani ndiyo inayompa mwananchi uhuru wa kuishi na kutembea popote nchini, kuanzia Mwanza, Mbeya hadi Tanga, bila hofu ya kutiliwa shaka au kuonekana mtu wa ajabu.

Nanga ameeleza kuwa taifa likiwa na amani, kila kitu kinafanyika vizuri na kwa utaratibu kwa sababu watu wanaheshimu sheria na kuzingatia maelekezo ya mamlaka. Amesema kuwa changamoto za kiusalama zikitokea, wananchi hukosa mambo mengi ya msingi, ikiwemo hata uwezo wa kufanya matembezi ya kawaida mitaani, jambo ambalo linathibitisha kuwa amani ni tunu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote ili kuliwezesha taifa kufika mbali.

Katika kutoa tahadhari, Nanga amewataka Watanzania kujifunza kupitia mataifa mengine duniani yanayopitia machafuko na kukosa utulivu, akisisitiza kuwa hali hiyo inaharibu mfumo wa maisha ya watu. 

Amesema kuwa sisi kama taifa tunapaswa kuendelea kuwa vinara wa kutunza amani yetu ili tuendelee kuishi kwa amani na mshikamano wakati wowote na mahali popote, tukizingatia kuwa amani ndiyo kitu pekee kinachotufanya tuishi vile tunavyotaka.