TANGAZO

TANGAZO

WAZIRI NDEJEMBI AWAKARIBISHA WABUNGE KUTEMBELEA KITUO CHA KUFUA UMEME CHA JULIUS NYERERE KIDIGITALI




-Awakaribisha kujionea kazi kubwa inayofanyika katika uzalishaji wa umeme

-Ni katika maonesho ya wiki ya nishati yanayoendelea Bungeni Dodoma

Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi amewakaribisha wabunge kutembelea Kituo cha kufua umeme cha Julius Nyerere ambacho kinazalisha jumla ya megawati 2115 za umeme kupitia kifaa maalumu cha uhalisia pepe. 


Mhe Ndejembi ameyasema hayo Aprili 20, 2026  wakati akikagua mabanda ya maonesho ya wiki ya nishati  yanayofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma yenye lengo la kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa  na taasisi chini ya Wizara ya Wizara ya nishati.

“Kupitia maonesho haya, wabunge watapata nafasi ya kujionea kazi mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Nishati kupitia taasisi zake. Hata ambaye hajawahi kufika katika Bwawa la Julius Nyerere ataweza kuliona kupitia teknolojia ya uhalisia pepe na kushuhudia juhudi kubwa zinazofanyika za kuzalisha umeme nchini,” alifafanua Mhe. Ndejembi.

Aidha, amewafahamisha wabunge kuwa wataalamu wa TANESCO kutoka mikoa mbalimbali wapo tayari kupokea na kushughulikia kero pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi katika majimbo yao, ili kuzitatua kwa haraka.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ameelezea juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amebainisha kuwa katika maonesho hayo, kuna majiko yanayotumia umeme kidogo ambayo yanaweza kupika chakula kwa ufanisi mkubwa.

“Katika maonesho haya, watu wataona jitihada zinazofanyika katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hapa kuna vyakula vinapikwa kwa kutumia nishati safi, mtajionea pia majiko ya kisasa yanayotumia umeme kidogo lakini yanapika kwa ufanisi ,” alisisitiza.

Maonesho ya Wiki ya Nishati yanafanyika kwa siku nne, huku bajeti ya Wizara ya Nishati ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni Aprili 22, 2026.