Vijana na wananchi kwa ujumla wametakiwa kutunza afya zao kwa kujiepusha na matumizi ya tumbaku, hususan sigara na shisha, kutokana na madhara makubwa kiafya yanayoweza kusababisha magonjwa ya moyo, matatizo ya mapafu na saratani.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, wakati wa uzinduzi wa taarifa ya mwaka 2025 kuhusu ushawishi wa kampuni za tumbaku katika sera za afya nchini.
Dkt. Kisenge alieleza kuwa matumizi ya tumbaku yanachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya ghafla, hasa kutokana na athari zake katika mishipa ya damu ya moyo. Aliongeza kuwa matumizi ya shisha, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi miongoni mwa vijana, ni hatari zaidi kwani kuvuta shisha mara moja kunaweza kuwa sawa na kuvuta sigara 100, hali inayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo na mgando wa damu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF), Lutgard Kokulinda Kagaruki, alisema tangu mwaka 2019 matumizi ya tumbaku nchini yameongezeka na kuifanya Tanzania kuwekwa katika kundi la tahadhari la alama nyekundu. Alisisitiza umuhimu wa serikali kufanya marekebisho ya sheria ya kudhibiti tumbaku ya mwaka 2003 ili iendane na changamoto za sasa na kudhibiti matumizi hayo.
Naye Dkt. Mwanaada Kilima alieleza kuwa gharama za matibabu ya magonjwa yanayosababishwa na tumbaku ni kubwa na mara nyingi huwaathiri vijana zaidi. Alibainisha kuwa mgonjwa mmoja anaweza kutumia zaidi ya shilingi milioni nne kwa mwaka kwa matibabu, jambo linaloleta hasara kwa taifa ikilinganishwa na faida ndogo inayotokana na uzalishaji wa tumbaku, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuacha au kupunguza matumizi yake.
