Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa mwito kwa Watanzania kutumia mafundisho ya dini kama nyenzo muhimu ya kutunza amani, umoja na mshikamano wa kitaifa ambao ndio utambulisho wa kipekee wa nchi yetu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA) la Musati mkoani Mara, Waziri Ulega amebainisha kuwa utofauti wa kidini nchini Tanzania ni tunu inayopaswa kuenziwa kwa kuwa inaleta upendo na maridhiano badala ya mifarakano.
Ametolea mfano mwaliko wake katika hafla hiyo ya kidini ya Aprili 19 kama kielelezo cha juu cha ukomavu wa Watanzania katika kuvumiliana na kupendana pasipo kujali imani zao, jambo linaloimarisha utulivu wa nchi.
Katika kutilia mkazo kampeni ya kitaifa ya maridhiano na mshikamano, Waziri Ulega ameeleza kuwa tofauti ya Tanzania na mataifa mengine ni namna ambavyo Watanzania wamekataa kugombanishwa na badala yake wamechagua kushikamana.
Alisisitiza kuwa mafundisho ya dini zote yanazungumzia umuhimu wa kupatana, kupendana na kumcha Mungu, mambo ambayo ndiyo msingi wa taifa kuwa salama.
Waziri alibainisha kuwa mshikamano huu wa kijamii ndio unaotoa fursa kwa serikali kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege mkoani Mara, ili kurahisisha huduma za usafirishaji na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Tukio hilo la uzinduzi wa kanisa lilihudhuriwa pia na viongozi waandamizi wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, jambo ambalo linaonyesha umoja wa viongozi katika kusimamia tunu za taifa.
Dkt. Nyansaho alieleza kuwa ujenzi wa kanisa hilo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 500 na litakuwa kituo cha huduma za kijamii kwa wote pasipo ubaguzi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alihitimisha kwa kushukuru ushirikiano unaoendelea kati ya viongozi na wananchi, akisisitiza kuwa ukarabati na uboreshaji wa mazingira ya watu unafanikiwa kwa sababu ya mazingira tulivu na yenye amani yaliyopo nchini.
