TANGAZO

TANGAZO

BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA KIBAHA LAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA JAMII KUPITIA ONGEZEKO LA MAKUSANYO YA MAPATO YA NDANI




Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha limeazimia kuendelea kuboresha huduma za jamii kwa wananchi kupitia matumizi sahihi ya mapato ya ndani yanayoendelea kuongezeka kutokana na juhudi za ukusanyaji wa mapato katika Manispaa hiyo.



Azimio hilo limefikiwa katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa robo ya tatu kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, ambapo wajumbe walijadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.



Katika kikao hicho, Baraza limekubaliana kuwa mafanikio ya ongezeko la makusanyo ya mapato yanapaswa kuonekana moja kwa moja katika maendeleo ya wananchi kwa kuimarisha huduma muhimu za kijamii zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi wa Manispaa ya Kibaha.

Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni huduma ya maji chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), ambapo Baraza limesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali ya Manispaa.

Aidha, Baraza limeelekeza hatua za haraka kuchukuliwa katika ukarabati wa miundombinu ya barabara chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), hususan barabara zilizoathirika kutokana na mvua nyingi za masika zinazoendelea katika kipindi hiki.

Akipokea taarifa katika Mkutano huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amesema amepokea mapendekezo hayo na atakaa pamoja na Timu ye Menejimenti kuchakata ili kupata namna bora ya kuboresha hali ya dharura ya kuharibika kwa miundombinu hiyo iliyosababishwa na mvua nyingi zinazoendela kunyesha katika kipindi hiki cha masika.

Katika sekta ya afya, Baraza limeweka mkazo katika kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya afya vya Manispaa, ikiwemo Kituo cha Afya Mwendapole, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye kukidhi mahitaji yao.

Vilevile, wajumbe wa Baraza wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha za mapato ya ndani ili kuhakikisha zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha katika kutekeleza uboreshaji wa miundombinu ya Barabara ndani ya Manispaa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imefanikiwa kupeleka kiasi cha shilingi milioni 420 kwa Kata zote 14 ikiwa ni kiasi cha shilingi milioni 30 kwa kila Kata, hata hivyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 700 kutoka mapato ya ndani ikiwa ni wastani wa shilingi milioni 50 kwa kila Kata ili kuendelea kuboresha hali ya miundombinu ya Barabara katika Manispaa hiyo.