Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali haitatoa tena ruzuku ya mishahara kwa Shirika la Reli Tanzania kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027 baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa ndani ya shirika hilo tangu mwaka 2017.
Profesa Mbarawa amesema hayo leo Jumatano Mei 13, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi bungeni jijini Dodoma.
Amesema Wizara inaishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuboresha TRC, zoezi ambalo lilianza rasmi mwaka 2017 kwa lengo la kuimarisha huduma za usafiri wa reli nchini pamoja na kuongeza ufanisi wa shirika hilo.
“Tangu kuanzishwa kwa Shirika hilo, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya mishahara. Naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 TRC haitatengewa tena ruzuku kwa ajili ya mishahara kutoka Serikalini,” amesema Profesa Mbarawa.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni ishara ya kuimarika kwa uwezo wa kifedha wa TRC kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya reli, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) pamoja na maboresho ya miundombinu ya reli nchini.
