TANGAZO

TANGAZO

TRILIONI 4.2 KULINDA MIPAKA: SERIKALI YAANIKA MKAKATI KABAMBE WA KUIMARISHA ULINZI WA TAIFA


Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) bungeni jijini Dodoma, Waziri Dk. Rhimo Nyansaho aliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi 4,286,489,115,000 kwa ajili ya Mwaka wa Fedha 2026/2027. 

Fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza maeneo manane ya kipaumbele yaliyopangwa kulinda mipaka ya nchi yenye urefu wa jumla ya kilometa 5,923.41 inayojumuisha ujirani na nchi kavu za Burundi, DRC, Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Uganda, na Zambia, pamoja na maili za baharini 864.376 kuelekea Comoro na Shelisheli ambapo kote hali ni shwari kabisa.

Katika kufanikisha azma hiyo, wizara imetaja kipaumbele chake cha kwanza kuwa ni kuliimarisha jeshi kwa kulipatia zana za kisasa, mifumo ya kiteknolojia, na mawasiliano ya uhakika, hususan wakati huu ambapo ulinzi wa anga la juu ukielezwa kuwa hautabiriki kutokana na kasi kubwa ya teknolojia duniani. 

Kipaumbele cha pili kinahusisha uboreshaji wa mazingira ya utendaji kazi wa wanajeshi kupitia utunzaji wa zana, mafunzo, maslahi, na makazi bora ili kukabiliana na changamoto za kiufundi mipakani ikiwemo uharibifu wa alama za mipakani na ukosefu wa barabara za ulinzi. 

Mkakati huu utasaidia pia kudhibiti athari za migogoro ya ndani ya majirani zetu, kama vile mapigano ya Mashariki mwa DRC ambapo kundi la M23 linashikilia miji ya kimkakati ya Goma, Bukavu, na Uvira, pamoja na tishio la kundi la kigaidi la Ansar Al-Sunna Wal Jamaah nchini Msumbiji karibu na mpaka wa Mtwara, ingawa maeneo hayo yote kwa upande wa Tanzania yameendelea kubaki salama.

Kipaumbele cha tatu na nne cha bajeti hiyo kimejikita katika kuimarisha miundombinu ya JKT ili kuchukua vijana wengi zaidi nchini kwa mafunzo ya uzalendo, kuliimarisha Jeshi la Akiba, na kulinda miradi yote ya kimkakati kwa maslahi ya taifa. 

Maeneo mengine ya vipaumbele ni pamoja na kuimarisha taasisi za utafiti wa kijeshi, kuanzisha viwanda vipya vya sekta ya ulinzi kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kiraia, na kushirikiana na sekta binafsi katika uwekezaji huo wa viwanda.

 Kipaumbele cha mwisho kinalenga kuimarisha diplomasia ya ulinzi na kikanda kupitia Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, SADC, na EAC, pamoja na kusaidia mamlaka za kiraia wakati wa majanga. 

Utekelezaji wa mpango huu mzito um kuzingatia kikamilifu miongozo mikuu ya nchi ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025.