TANGAZO

TANGAZO

MWENYEKITI WA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA NA WADAU WAHIMIZA MARIDHIANO BILA MASHARTI


Akitoa darasa kuhusu umuhimu wa hatua hiyo, Khatibu alisisitiza kuwa nchi inaelekea kwenye maridhiano ili kutatua changamoto, kuondoa mizozo, na kuzuia kujirudia kwa vurugu zilizoshuhudiwa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.



Alionya wanasiasa dhidi ya kuweka masharti magumu yanayoweza kukwamisha mchakato huo, akitolea mfano wa mchakato wa katiba pendekezwa wa mwaka 2014 ulivyokwama baada ya baadhi ya wanasiasa kujitoa, na kuwasihi kuweka pembeni malengo ya vyama vyao ili kuiponya nchi kwani Tanzania imekuwa kimbilio la amani kwa mataifa yenye migogoro.

Nia ya kuundwa kwa tume hii ya maridhiano si jambo lililokuja kwa kushurutishwa na mazingira magumu ya uchaguzi uliopita, bali lilikuwa sehemu ya mpango wa mapema wa serikali.

Rais Samia Suluhu Hassan alithibitisha ukweli huo kupitia hotuba yake aliyoitoa tarehe 23 Aprili mwaka huu baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Rais Samia alieleza kuwa kuundwa kwa tume hiyo ilikuwa miongoni mwa ahadi zake za siku 100 za kwanza tangu aingie madarakani, lakini utekelezaji ukacheleweshwa na ghasia zilizojitokeza, akiahidi kuwa hivi karibuni itaundwa tume jumuishi itakayokusanya wadau wote muhimu ili kuziba mianya ya migawanyiko na kurejesha umoja wa kitaifa baada ya serikali kufanya tathmini ya kina ya mapendekezo yaliyowasilishwa.

Umuhimu wa ushirikishwaji mpana katika tume hiyo umeungwa mkono kwa nguvu zote na Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ambaye pia alikuwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2025 kupitia chama hicho.

Mwalimu alisisitiza kuwa makundi yote yenye ushawishi na uwezo wa kubeba maono ya Watanzania yanapaswa kuhusishwa kadiri isivyofikirika na kupewa uhuru wa kujadili mambo yote yaliyopendekezwa na tume ya Jaji Chande, pamoja na yale yaliyokuwa nje ya hadidu za rejea.

Alibainisha kuwa mambo yote yanayohitajika kurudisha mshikamano wa taifa yasizuiwe kujadiliwa kwa sababu kuzungumza wazi ndiko kunakoleta uponyaji wa dhati kwa jamii iliyoumia.

Naye Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk. Ahmad Sovu, alifafanua kuwa ili kuwafikia Watanzania wote, tume hiyo lazima ijumuishe vijana, wataalamu wa sheria, wanasaikolojia, wataalamu wa utawala bora, haki za binadamu, na waathirika wa ghasia za uchaguzi wa Oktoba 2025.

Dk. Sovu alitahadharisha kuwa kuna baadhi ya viongozi wa siasa wenye tabia ya 'nongwa' wanaweza kutumia mchakato huo kunyoshea wengine vidole kwa maslahi binafsi, hivyo akashauri wajumbe watakaoteuliwa wawe watu waaminifu, wasioegemea upande wowote, na wenye rekodi nzuri ya kutetea ukweli bila uoga.