![]() |
Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu katika mikoa ya Arusha, Iringa na Mbeya kwa tuhuma za kutumia mitandao ya kijamii vibaya, ikiwemo kutoa matusi na lugha za kashfa dhidi ya wajumbe wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya vurugu za Oktoba 29, 2025. Hatua hiyo imekuja ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi katika kudhibiti vitendo vya utapeli, udhalilishaji na matusi dhidi ya viongozi na wananchi kwa ujumla, kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Taarifa kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dodoma imebainisha kuwa hali ya usalama wa nchi ni shwari, licha ya kuwepo kwa kundi dogo la watu wanaoendelea kutumia vibaya majukwaa ya kidijitali kupanda mbegu za chuki na uchochezi.
Jeshi la Polisi limepata mafanikio hayo kutokana na ushirikiano wa karibu na wananchi pamoja na wadau wengine ambao wamekuwa mstari wa mbele kubaini na kuzuia uhalifu kabla haujaleta madhara makubwa kwenye jamii.
Kwa sasa, Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali wa kuwasaka watuhumiwa wengine wanaojihusisha na uandishi wa jumbe za matusi, kashfa, na uchonganishi unaolenga kupandikiza chuki na upotoshaji wa makusudi.
Pia Jeshi la Polisi limewataka wanaopokea jumbe hizo kutoka kwa wahalifu na kuendelea kuzisambaza, kuacha kufanya hivyo kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria na watachukuliwa hatua kali kama wahalifu wengine pindi watakapotiwa mbaroni.
Jeshi la Polisi limetoa shukrani za dhati kwa wananchi wazalendo wanaoendelea kutoa taarifa za siri zinazofanikisha kukamatwa kwa wanaokiuka Sheria ya Makosa ya Mtandaoni na sheria nyingine za nchi.
Jeshi limesisitiza kuwa litaendelea kuwachukulia hatua stahiki wote wanaotumia vibaya uhuru wa kutoa maoni kwa kudhalilisha wengine, ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu vilivyopo nchini vinaendelea kulindwa kwa gharama yoyote.
