TANGAZO

TANGAZO

WAZIRI MKUU ATATUA MGOGORO WA ARDHI ULIODUMU KWA MIAKA 51 WILAYANI ROMBO

 



Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ametatua mgogoro wa ardhi kati ya Parokia ya Mtimhoo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi na Mzee Peter Morisi wa Kijiji cha Msaranga, Wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, uliodumu kwa kipindi cha miaka 51.


Waziri Mkuu alipokea malalamiko ya Mzee Peter Morisi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro tarehe 17 Februari 2026 ambapo aliahidi kuwa Serikali ingetuma wataalamu wilayani humo kwa ajili ya kuchunguza na kutatua mgogoro huo.

Kufuatia maelekezo hayo, Waziri Mkuu alituma timu ya wataalamu kutoka Ofisi yake ambao walifika mkoani Kilimanjaro na kushirikiana na viongozi wa Mkoa pamoja na viongozi wa Kijiji cha Msaranga kutembelea eneo la mgogoro. Aidha, timu hiyo ilifanya vikao na familia iliyokuwa katika mgogoro, viongozi wa kijiji, viongozi wa Parokia ya Mtimhoo pamoja na viongozi wa Jimbo Katoliki la Moshi ambapo pande zote zilikubaliana kuwa maridhiano ndiyo njia sahihi ya kumaliza mgogoro huo.

Katika madai yake, Mzee Peter Morisi alieleza kuwa eneo lake lilichukuliwa kwa nguvu na Kanisa Katoliki na kwamba fidia aliyolipwa ilikuwa ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa eneo lililotwaliwa. Kutokana na kutopata suluhisho kwa muda mrefu, aliamua kuwasilisha malalamiko yake kwa Waziri Mkuu wakati wa mkutano wa hadhara.

Timu ya wataalamu ilipitia nyaraka zote zilizowasilishwa na pande husika na kubaini kuwa Mzee Peter Morisi alipokea fidia ya shilingi 3,935.50 tarehe 16 Aprili 1980. Aidha, alipewa eneo jingine katika Kitongoji cha Kirachi, Kijiji cha Msaranga ili kupisha ujenzi wa shule na kanisa katika eneo lake la awali.

Katika hatua nyingine, timu hiyo ilikutana na Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Askofu Ludovick Minde ambaye alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki lina utamaduni wa kutatua migogoro kwa njia ya maridhiano na kuwataka wahusika kuendelea na mazungumzo ya amani.

Askofu Minde alitoa shilingi milioni tano kama kifuta machozi kwa madhara ambayo Mzee Peter Morisi na familia yake wameyapitia katika kipindi chote cha kutafuta suluhisho la mgogoro huo. Aidha, alisema Kanisa halina kinyongo na mlalamikaji na litaendelea kushirikiana naye wakati wote.

Vilevile, Askofu Minde alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutuma timu ya wataalamu kutoka Ofisini kwake na kumtakia heri katika utekelezaji wa majukumu yake ya uongozi.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Waziri Mkuu naye alitoa shilingi milioni tano na kufanya jumla ya fedha zilizotolewa kwa Mzee Peter Morisi kuwa shilingi milioni kumi kwa lengo la kujenga maridhiano na kuimarisha mshikamano katika jamii.

Baada ya kufikiwa kwa maridhiano hayo, pande zote zilitia saini nyaraka za makubaliano zikikiri kuwa mgogoro huo umemalizika kwa njia ya maridhiano na kuahidi kusameheana pamoja na kuendelea kuishi kwa amani. Kila upande pia ulikabidhiwa Hati za Hatimiliki za Kimila kwa maeneo husika.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa hati hizo na kusaini nyaraka za maridhiano, Mzee Peter Morisi aliishukuru Serikali kwa kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu na kuahidi kushirikiana na Kanisa pamoja na wanakijiji wenzake bila kinyongo.

Naye Diwani wa Kata ya Kisale Msaranga, Mhandisi Mathias Assenga alisema mgogoro huo uliathiri mshikamano wa wananchi pamoja na uhuru wa kuabudu kwa kuwa ulihusisha eneo la kanisa linalotumiwa na waumini kwa ibada na shughuli nyingine za kidini.

Kwa upande wake, Padri Amadeus Mtui ambaye ni Wakili wa Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutuma timu ya wataalamu ambayo imekuwa chachu ya kumalizika kwa mgogoro huo.

Baadhi ya viongozi walioshiriki katika mchakato wa maridhiano hayo ni pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Charles Daudi Mganga, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kilimanjaro, Rehema Mdee pamoja na Diwani wa Kata ya Kisale Msaranga, Mhandisi Mathias Assenga.

Mzee wa Kijiji cha Msaranga, Andrea Peter Mkenda alisema kumalizika kwa mgogoro huo kutaleta amani, utulivu na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wananchi hali itakayowapa nafasi nzuri ya kuendelea na shughuli zao za maendeleo.