Wauguzi na Wakunga nchini, wametakiwa kuzingatia utu, staha na mawasiliano mazuri kati ya watoa huduma na wananchi ili wagonjwa waweze kuelewa hali zao za kiafya, dawa wanazotumia pamoja na huduma wanazopaswa kuendelea kupata hata baada ya kutoka hospitalini.
Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah ametoa rai hiyo Mei 20, 2026 kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wauguzi viongozi unaofanyika katika kumbi za PSSF mkoani Dodoma.
"Wauguzi wanatoa takriban asilimia 80 ya huduma zote za afya, hivyo ni muhimu kuendelea kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa bora na zenye kukidhi mahitaji ya wananchi," amesema Bi. Ziada
Amesema, lengo la mkutano huo muhimu ni pamoja na kufanya tathmini ya huduma za afya zinazotolewa katika vituo mbalimbali, kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kubadilishana uzoefu.
Aidha, Bi. Ziada amesema kuwa utaratibu wa viongozi hao kukutana kila mwaka unalenga kufanya tathmini ya huduma zinazotolewa kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali ya Taifa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi.
"Pamoja na tathmini hiyo, viongozi hawa pia hupata taarifa na maboresho mbalimbali yanayotolewa na Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani WHO kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma katika vituo vya kutolea huduma nchini," amesema Bi. Ziada.
Kwa upande wa wananchi Bi. Ziada amewahimiza kutoa taarifa mapema wanapokutana na changamoto katika huduma za afya ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati, huku akiwataka wanawake wajawazito kuwahi kliniki mapema ili wataalamu waweze kubaini changamoto zozote za kiafya na kuzipatia ufumbuzi mapema.
Mkutano huo umewakutanisha wauguzi viongozi wa mikoa, halmashauri, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za kanda, hospitali za taifa pamoja na waratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto kutoka maeneo mbalimbali nchini.




