Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha malezi na makuzi ya watoto, kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi pamoja na kujenga familia imara, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuharakisha maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo Julai 4, 2026 wakati akifungua Kongamano la Usiku wa Mtoko wa Familia lililoandaliwa na Rizex for Life Foundation katika Ukumbi wa Bombambili, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ambapo pamoja na kutoa elimu ya malezi na makuzi ya watoto, taasisi hiyo imefadhili vijana 10, wakiwemo wasichana watano na wavulana watano, kujiunga na masomo ya ufundi stadi katika Chuo cha VETA.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi yanayowezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kushirikiana na Serikali katika kuimarisha ustawi wa familia, kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi pamoja na kuleta maendeleo endelevu ya jamii.
"Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha malezi ya watoto, kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi na kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi na Serikali tutaendelea kutekeleza Sera, Sheria na Programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha malezi ya watoto na ustawi wa familia, wazazi na walezi mnapaswa kuwa karibu na watoto wenu ili kuwajengea maadili mema, kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwalea katika misingi ya uzalendo na uwajibikaji.," amesema Naibu Waziri Mahundi.
Aidha, ameipongeza Rizex for Life Foundation kwa kuendelea kugusa maisha ya vijana kupitia ufadhili wa elimu ya ufundi stadi na kutoa elimu ya malezi bora kwa familia, hatua ambayo amesema inaunga mkono juhudi za Serikali za kujenga rasilimali watu yenye tija.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema familia ndiyo msingi wa jamii imara na kwamba amani, maadili, mshikamano na uzalendo huanzia ndani ya familia, hivyo elimu inayotolewa kupitia kongamano hilo ni uwekezaji muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha, amewahimiza wazazi, walezi na vijana kutumia elimu waliyoipata kupitia kongamano hilo kujenga familia zenye mshikamano, kudumisha maadili mema na kuendelea kuenzi amani, umoja na upendo, huku akiipongeza Rizex for Life Foundation kwa mchango wake katika kuelimisha jamii na kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo ya wananchi.




