TANGAZO

TANGAZO

MJI WA SERIKALI MTUMBA KUWA MFANO WA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KUPITIA GESI ASILIA



Imeelezwa kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya kuufanya Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kuwa mfano wa matumizi ya nishati safi kupitia mradi wa usambazaji wa gesi asilia.


Miundombinu hiyo itaunganisha  gesi asilia katika majengo ya Wizara, ofisi za Ubalozi, taasisi za Serikali, majengo ya biashara, hoteli, migahawa pamoja na makazi ya eneo la Mtumba.


Hayo yameelezwa na Mjiolojia kutoka Wizara ya Nishati, Nuru Helambili  wakati akitoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba). 


Helambili amesema mradi huo unalenga kujenga kituo cha kupokelea gesi (Gas receiving terminal) itakayokuwa ikisafirishwa kwa magari maalum kutoka Kituo Mama cha CNG kilichopo Mlimani City, Dar es Salaam.


Amefafanua kuwa mradi huo utahusisha pia ujenzi wa kituo cha kupunguza mgandamizo wa gesi, mtandao wa usambazaji na kituo cha kujazia gesi asilia kwenye magari. 


Helambili ameeleza kuwa  katika mwaka 2026/2027  Serikali itakamilisha tathmini ya athari kwa mazingira na jamii na kuanza taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likitenga shilingi bilioni 14.40 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo.