Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonya makundi yanayojificha nyuma ya mwamvuli wa uanaharakati na uzalendo, huku kiuhalisia yanajihusisha na uchochezi, vurugu na vitendo vya kigaidi vyenye lengo la kuvuruga amani na usalama wa taifa.
Akizungumza katika hafla ya kihistoria ya utiaji saini wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo iliyofanyika katika Viwanja vya Ikulu, Zanzibar, Julai 9, 2026, Rais Samia amesisitiza kuwa usalama wa nchi na utulivu wa wananchi ni mambo yasiyo na mjadala wala mbadala, na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kuchezea misingi hiyo mikuu.
“Niwaonye wanaojishughulisha na vitendo vya kigaidi, Taifa lolote duniani hutumia nguvu ya dola kuhami raia wake na kulinda heshima yake, nasi Tanzania hatutasita kufanya hivyo,” amesema Rais Samia.
Katika hotuba yake hiyo nzito iliyobeba mwelekeo wa kitaifa, Rais Samia amefafanua kuwa ugaidi unajumuisha vitendo vyote vya uvunjifu mkubwa wa amani, uharibifu wa mali na miundombinu ya umma, ambavyo vinalenga kuitishia jamii au kuishurutisha na kuishinikiza Serikali kupitia njia zisizo halali ili kutekeleza matakwa ya kundi au watu fulani kwa maslahi ya kisiasa, kiitikadi au kidini.
Rais Samia ameweka wazi kuwa baadhi ya makundi duniani yamekuwa yakitumia mbinu hizi za kigaidi kama nyenzo ya kuzikwamisha nchi zinazopiga hatua kubwa za maendeleo, huku wahusika wakijivika ngozi ya kondoo na kujionyesha kuwa wazalendo ilhali malengo yao makuu ni kupanda mbegu ya chuki na kusambaratisha utulivu wa mataifa.
Dkt. Samia amewakumbusha wananchi kuwa uzalendo wa kweli haupimwi kwa kuichafua, kuivuruga au kuiharibu nchi, bali unaonyeshwa kwa vitendo vya kulinda amani, kuheshimu sheria na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Nataka niwaonye wale wote wanaojiita wanaharakati, lakini matendo yao yanaathiri amani ya nchi kwa kujihusisha na vurugu, uharibifu wa mali na miundombinu kwa lengo la kutimiza ajenda zao za kisiasa au kiitikadi,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesisitiza kuwa uzalendo wa kweli hauonyeshwi kwa kuichafua au kuiharibu nchi, bali kwa kulinda amani, kuheshimu sheria na kushiriki katika kujenga maendeleo.
Amewakumbusha kuwa hata pale viongozi walipokuwa na tofauti za kisiasa, walichagua njia ya mazungumzo badala ya migogoro na machafuko, jambo lililowezesha Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani.
“Aneyeipenda nchi yake hawezi kuiweka katika mazingira ya vurugu. Tofauti zetu zinapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo na kuheshimiana, si kwa vitisho wala uharibifu,” amesema.
Ameongeza kuwa hata pale viongozi wa kisiasa wanapokuwa na mitazamo au tofauti kubwa, daima wamekuwa wakichagua njia ya uungwana ya mazungumzo na maridhiano badala ya migogoro na machafuko, jambo lililowezesha Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha utulivu.
Dkt. Samia amesema matarajio makubwa ya wananchi ni kuona upatikanaji wa huduma bora za kijamii, ustawi wa maisha, ukuaji wa uchumi na fursa za ajira.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa siasa za chuki na mivutano huathiri maendeleo, wakati siasa za staha, maridhiano na kuheshimiana hujenga umoja, kuimarisha ustawi wa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Amebainisha kuwa kwenye siasa za chuki maendeleo hutoweka, lakini kwenye siasa za staha, utu, heshima na maridhiano kama yale yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT-Wazalendo, maendeleo yanapata nafasi ya kuchanua.
Amewahakikishia Watanzania kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa uimara wa hali ya juu na bila kuyumba, huku akiwasihi wananchi kushikamana, kutanguliza maslahi mapana ya taifa mbele, na kushirikiana na Serikali kulinda amani ili Mwenyezi Mungu alijalie taifa hekima na unyenyekevu katika kulinda makubaliano hayo kwa manufaa ya Zanzibar na Tanzania nzima.
Katika hotuba yake baada ya kusainiwa kwa maridhiano hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, amesema kusainiwa kwa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar ni hatua ya kihistoria yenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha amani, mshikamano na ustawi wa wananchi wa Zanzibar na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mwinyi amesema ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni msingi wa kuleta maendeleo endelevu.
Amewahimiza wananchi na viongozi kuendelea kushirikiana katika kulinda mafanikio ya maridhiano hayo, akieleza kuwa Serikali itaendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wa mchakato huo kupitia ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili.







