Ushiriki mkubwa umeshuhudiwa katika Tuzo za Samia Kalam Awards 2026 baada ya waandishi wa habari na maafisa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini kuwasilisha jumla ya kazi zao kwa ajili ya kushindanishwa.
Kazi hizo ni zile ambazo washiriki walizirusha hewani na kuzichapisha kupitia vyombo vyao vya habari, kwa kuzingatia muongozo uliotolewa na waandaaji wa tuzo hizo.
Akizungumza leo Novemba 17, 2026 kuhusu mwenendo wa tuzo hizo, Mkuu wa idara ya Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma, Bw. Rolf Kibaja, amesema tuzo hizo zimeendelea kutoa fursa muhimu kwa waandishi wa habari na maafisa habari kuonesha ubora wa kazi zao na mchango wao katika jamii.
Amesema ushiriki huo mkubwa unaonesha jinsi wadau wa habari wanavyozithamini tuzo hizo na dhamira yao ya kuendelea kukuza taaluma ya habari nchini.
"Tuzo hizi zinatoa fursa kwa waandishi wa habari na maafisa habari kushindanisha kazi walizozirusha hewani, katika muongozo wa tuzo. Ushiriki wao pamoja na mwitikio wa wananchi unaonesha thamani kubwa ya tuzo hizi," amesema Bw. Kibaja.
Kibaja ameongeza kuwa mwitikio wa wananchi kwa tuzo hizo umeendelea kukua, jambo linalodhihirisha kuwa kazi za waandishi wa habari zinaendelea kugusa maisha ya wananchi na kuchangia katika kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.
![]() |
Ameeleza kuwa kupitia tuzo hizo, waandaaji wanalenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha ubora, weledi, uadilifu na uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya habari.
Kwa mujibu wake, tuzo hizo pia ni chachu ya kuwawezesha waandishi wa habari kuendelea kuboresha kazi zao, kufanya uchunguzi wa kina na kutoa habari sahihi, zenye uwiano na zinazozingatia maslahi ya umma.
Tuzo za Samia Kalam Awards ni miongoni mwa tuzo muhimu nchini zinazolenga kutambua mchango mkubwa wa sekta ya habari katika kujenga uelewa wa wananchi, kukuza demokrasia na kuhamasisha maendeleo ya Taifa.
Hafla ya kuwatunuku Washindi itafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam Disemba 5, 2026 huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.











