TANGAZO

TANGAZO

TUTUMIE AFCON KAMA FURSA YA KUJITANGAZA KIMATAIFA - DKT. YONAZI




Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ya Maandalizi ya Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027),  Dkt. Jim Yonazi, amesema michuano ya AFCON ni fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania Kimataifa kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii na uwekezaji hivyo ni jukumu la kila sekta kuhakikisha inachangamkia na kushiriki kikamilifu katika kufanikisha michuano hiyo.






Ameyasema hayo hii leo 01 Julai 2026 wakati wa ziara ya Kamati hiyo inayojumuisha Makatibu Wakuu wa kisekta na baadhi ya wakuu wa Taasisi walipotembelea na kukagua maendeleo ya maandalizi kuelekea michuano hiyo ikiwemo kuangalia miundombinu na vituo vya michezo vitakavyotumika katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027) ili kufanikisha mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.


Katika ziara hiyo, Kamati imekagua maendeleo ya maboresho katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Uwanja wa Mazoezi wa Shule ya Sheria (Law School Grounds), Uwanja wa Mazoezi wa Leaders Club, Uwanja wa Mazoezi wa Gymkhana (Gymkhana Club), Uwanja wa Mazoezi wa Farasi pamoja na Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa ili kujionea utayari wa miundombinu itakayotumika wakati wa mashindano hayo.


Dkt. Yonazi amesema ili kufanikisha AFCON 2027 kila sekta inapaswa kuweka nguvu ya pamoja katika kuelekea kwenye michuano hiyo kwa kuzingatia faida zake ikiwemo ya kukuza uchumi wa jamii na Nchi kwa ujumla  


"AFCON 2027 ni zaidi ya mashindano ya soka; ni jukwaa la kuitangaza Tanzania Duniani hivyo kila taasisi inapaswa kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha nchi inanufaika ipasavyo na fursa hii," amesema Dkt. Yonazi.


Aidha, ameielekeza Bodi ya Utaliii Tanzania (TTB) kuandaa mkakati mahsusi wa kuitangaza Tanzania kupitia mashindano hayo kwa kuonesha vivutio vya utalii, utamaduni na fursa za uwekezaji kwa wageni watakaofika nchini.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeelo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Boniface Tamba, amesema maboresho ya miundombinu yanaendelea vizuri na kwamba ujenzi wa barabara zinazoingia na kutoka katika vituo pamoja na viwanja vya michezo umefikia hatua za mwisho za ukamilishaji.


"Maandalizi yanaendelea kwa kasi na miundombinu muhimu ipo katika hatua za mwisho ili kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kuandaa AFCON 2027 kwa viwango vinavyotakiwa," amesema Bw. Tamba.


Kamati ya Makatibu Wakuu inaendelea na ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya AFCON 2027, ambapo baada ya kukamilisha ukaguzi katika Mkoa wa Dar es Salaam itatembelea Zanzibar kabla ya kuhitimisha ziara hiyo itatembelea katika viwanja vilivyopo  Jijini Arusha.