-Wadau watakiwa kujiandaa mapema kabla masoko ya dunia hayajawalazimisha kubadilika
Serikali ya Tanzania imewataka wadau wa sekta ya almasi nchini kuhakikisha almasi ya Tanzania haiuzwi kwa ubora wa jiwe pekee, bali pia kwa ushahidi kwamba ilichimbwa na kuuzwa kwa kuzingatia sheria, mazingira, haki za binadamu na uadilifu.
Wito umetolewa leo Septemba 24, 2026 na Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, mkoani Shinyanga wakati akifungua Mkutano wa Uhamasishaji kuhusu Kiwango cha Almasi Endelevu (Sustainable Diamond Standard - SDS) kilichoandaliwa na Chama cha Nchi za Afrika Zinazozalisha Almasi (ADPA).
"Ujumbe wetu ni mmoja: tunataka almasi inayozalishwa Tanzania iwe na thamani katika jiwe lenyewe, lakini pia iwe na thamani katika namna ilivyozalishwa na kuuzwa," amesema Dkt. Mwanga.
Dkt. Mwanga amesema kwa sasa ubora na thamani ya almasi pekee haitoshi, wanunuzi, wawekezaji na masoko ya kimataifa wanataka uhakika kwamba almasi imezalishwa kwa kuzingatia afya na usalama kazini, maslahi ya jamii na uadilifu katika biashara. SDS, amesema, imeandaliwa kuweka kiwango cha pamoja cha uchimbaji na biashara ya almasi ghafi yenye uwajibikaji, na kuboresha utendaji wa kampuni katika mazingira, jamii na utawala bora.
"Hatupaswi kusubiri mahitaji ya masoko ya kimataifa yatulazimishe kubadilika; tunapaswa kujiandaa mapema na kujenga mifumo itakayowezesha almasi ya Tanzania kuendelea kuaminika na kushindana katika masoko ya dunia," amesisitiza Dkt. Mwanga.
Dkt. Mwanga amesema uchimbaji endelevu si jambo jipya nchini. Sheria ya Madini, Sura ya 123, na Kanuni zake tayari zinasimamia utafutaji, uchimbaji, uchakataji na biashara ya madini. Sheria hiyo pia inazingatia mazingira, afya na usalama, ushiriki wa Watanzania (local content), uwajibikaji kwa jamii na uzingatiaji wa sheria. Kwa msingi huo, amesema, sheria za Tanzania zinaendana kwa kiwango kikubwa na madhumuni ya SDS.
"SDS haipaswi kuonekana kama mbadala wa Sheria ya Madini ya Tanzania, bali kama fursa ya kuimarisha na kuonesha kwa masoko ya kimataifa utekelezaji wa viwango vya uwajibikaji vinavyotakiwa katika mnyororo wa thamani wa almasi," amesema Mwanga.
Ameeleza kuwa Serikali itafanya tathmini ya kina kulinganisha SDS na Sheria ya Madini ili kubaini maeneo yanayokidhiwa tayari, yanayohitaji kuimarishwa, na yanayohitaji mwongozo wa ziada. Lengo ni kuhakikisha utekelezaji wa kiwango hicho unakuwa wa vitendo na wenye manufaa kwa Taifa.
Dkt. Mwanga amesema uwazi, uadilifu na ufuatiliaji wa chanzo cha madini ni muhimu katika kulinda taswira ya Tanzania. Mfumo wa nchi wa kusimamia uzalishaji, uhifadhi, uthamini na biashara ya madini, pamoja na matakwa ya Mchakato wa Kimberley (Kimberley Process), tayari unatoa msingi imara wa biashara halali ya almasi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwanga, SDS inaweka utaratibu wa kujitathmini, kuhakikiwa na mtoa huduma huru, na hatimaye kupata cheti (certification). Watakaokidhi masharti wataruhusiwa kutumia Sustainable Diamond Logo kwenye bidhaa zao, alama inayotarajiwa kuongeza imani ya wanunuzi duniani.
Kiwango hicho kinawatambua washiriki wote katika mnyororo wa thamani, wakiwemo wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo pamoja na wafanyabiashara. Dkt. Mwanga amesisitiza kuwa utekelezaji wake lazima uende sambamba na ajira na mafunzo kwa Watanzania, uhamishaji wa teknolojia, ushiriki wa wafanyabiashara wa ndani, na maendeleo ya jamii zinazozunguka migodi. Ametaka pia wachimbaji na wafanyabiashara wadogo waelimishwe ili washiriki kikamilifu katika biashara rasmi ya almasi.
ADPA ilianzishwa tarehe 4 Novemba 2006 kupitia Azimio la Luanda na makao yake makuu yako Luanda, Angola. Ina wanachama kamili 15, ikiwemo Tanzania, na waangalizi saba.
Kikao cha Shinyanga kimewaleta pamoja wadau wa mnyororo wa thamani wa almasi kujadili madhumuni, wigo, muundo na viwango vya SDS, pamoja na Sheria ya Madini ya Tanzania.







