TANGAZO

TANGAZO

UMEME JUA KISHAPU AWAMU YA PILI KUIONGEZEA TANZANIA MEGAWATI 100 ZA NISHATI JADIDIFU








 -Waziri Ndejembi ashuhudia utiaji saini, asema ni alama ya miradi ya kielelezo nchini.

-Mradi utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 100

 -Aeleza mradi kugharimu Shilingi bilioni 204.4 na kuchochea sekta za kilimo, viwanda na uchimbaji wa madini.

 -Aitaka TANESCO kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi ili ukamilike kwa wakati.

 

Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeingia hatua mpya ya kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme baada ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa umeme kwa nguvu ya Jua Kishapu utakaozalisha jumla ya megawati 100.

 




Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 50 na kuingizwa katika Gridi ya Taifa, jambo lililoongeza uwezo na uthabiti wa gridi hiyo na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Akizungumza katika hafla hiyo Julai 27, 2026, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema sekta ya nishati ni mhimili wa maendeleo ya Taifa ambapo Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuongeza vyanzo mseto vya uzalishaji wa umeme (Energy Mix) ili kuhakikisha Tanzania haitegemei chanzo kimoja pekee cha uzalishaji wa umeme.

 

"Wananchi wa maeneo haya walikuwa wanategemea umeme uliokuwa unasafirishwa kutoka umbali mrefu. Kukamilika kwa mradi huu kutaifanya Tanzania kuwa na mfumo salama zaidi wa umeme na kuwa nchi ya mfano katika uzalishaji wa umeme unaostahimili mabadiliko ya tabianchi," amefafanua Mhe. Ndejembi.

 

Aidha, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia ufadhili wa mkopo wenye masharti nafuu. Amesema ushirikiano huo unaonesha imani kubwa ya washirika wa maendeleo katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini.

 

Pia ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme inayobadili taswira ya sekta ya nishati nchini, huku akiitaka kuhakikisha mradi huo unasimamiwa kwa karibu katika kila hatua ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuanza kuwanufaisha wananchi.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesema utekelezaji wa mradi huo unaonesha  dhahiri dhamira ya Wizara ya Nishati ya kuelekeza asilimia 97 ya bajeti yake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

"Hatua hii ya utiaji saini ni matokeo ya diplomasia nzuri ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyowafanya washirika wetu wa maendeleo kuendelea kuiamini Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme. Tunaamini Tanzania itaendelea kuwa na umeme wa kutosha," amesisitiza Mhe. Mgalu.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Mhe. Balozi Zuhura Bundala, amesema Bodi ilisimamia kwa karibu utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo na kuridhishwa na namna ulivyotekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyowekezwa. Amesema utiaji saini wa awamu ya pili ni hatua nyingine muhimu inayodhihirisha mafanikio ya mradi huo.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema gharama za mradi mzima wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150 ni takribani Shilingi bilioni 323. Kati ya fedha hizo, awamu ya kwanza yenye uwezo wa kuzalisha megawati 50 imegharimu Shilingi bilioni 118.6, huku awamu ya pili yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 ikitarajiwa kugharimu takribani Shilingi bilioni 204.4.

 

"Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 17 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TANESCO na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ambalo limetoa mkopo wenye masharti nafuu," amefafanua Bw. Twange.

 

Mkataba huo umesainiwa kati ya TANESCO na muungano wa makampuni mbili kutoka Ufaransa na Tunisia, ambayo ni Sagemcom Energy, Telecom SAS na STEG International Services.