Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro Abdul-Razaq Badru ameuambia mkutano wa 48 wa kamati ya Urithi wa Dunia kuwa Ngorongoro ni sehemu pekee ambayo binadamu duniani kote wanaweza kupata ushahidi sahihi wa chimbuko la asili ya binadamu.
Akizungumza mjini Busan,Jamhuri ya Korea wakati akiongoza Mkutano wa pembeni (Side event) ulioandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja kuhusu hali ya uhifadhi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni eneo la Urithi wa Dunia, Badru amesema Ngorongoro ina ushahidi uliohifadhiwa wa nyayo za binadamu na masalia ya kale katika eneo la Laetoli na Olduvai zinazothibitisha suala hilo.
“Ngorongoro si tu eneo la utalii bali pia ni mahali ambapo historia ya binadamu wote kisayansi ilianzia”, alisema kamishna Badru.
Katika kikao hicho ameeleza kuwa kila nyayo iliyohifadhiwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro inawakumbusha kurudi nyumbani kuona historia hiyo.
Badru amefafanua kuwa Ngorongoro ni sehemu ambayo binadamu alianzia kutumia zana mbalimbali za mawe kama teknolojia ya awali ya shughuli za kibinadamu na ndipo alipoanza kufanya harakati za kimaisha.
Mkutano wa kamati ya Urithi wa Dunia una lengo la kufanya maamuzi kuhusu maeneo mapya yanayopendekezwa kuingizwa kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia na kuimarisha juhudi za pamoja za kulinda, kuhifadhi, na kusimamia kwa uendelevu maeneo yenye thamani kubwa ya kiutamaduni na asili duniani.


