WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania, taasisi za umma na binafsi, mashirika na wadau wa maendeleo waungane na Serikali katika kuwezesha matibabu ya upandikizaji wa figo na uloto kwa wananchi wasiokuwa na uwezo ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hizo za kibingwa.
"Hiki ni kitendo cha kiungwana, cha ibada na kinachogusa maisha ya Watanzania. Nawapongeza Umoja wa Wanawake Tanzania kwa kuitikia wito huu na kuwa sehemu ya kuokoa maisha ya wananchi," amesema.
"Tunachokifanya leo ni kurejesha matumaini kwa wagonjwa na familia zao. Kila anayeguswa na jambo hili aendelee kushiriki ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hizi muhimu," amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo jana (Alhamisi, Julai 16, 2026) katika hafla ya Okoa Maisha Gala iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa katika Ukumbi wa Mabele Hall, Jenerali Venance Mabeyo Complex, jijini Dodoma.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu, kuongeza vifaa tiba na kuimarisha huduma za kibingwa ili Watanzania wengi zaidi wapate matibabu ya kiwango cha juu ndani ya nchi.
Awali, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema Serikali itaendelea kuboresha huduma za kibingwa nchini kwa kuimarisha miundombinu ya afya, vifaa tiba na rasilimali watu, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono Mfuko wa Matibabu ya Upandikizaji wa Figo na Uloto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, alisema hospitali hiyo imefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 58 na upandikizaji wa uloto kwa watoto 31 wenye ugonjwa wa selimundu. Alisema kampeni hiyo inalenga kukusanya shilingi bilioni saba kwa ajili ya kusaidia matibabu ya wagonjwa na kupanua miundombinu ya huduma hizo.
Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Pius Chatanda, alisema umoja huo utaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha wadau na wananchi kushiriki katika juhudi za kuokoa maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa huduma bora za afya.
Katika hafla hiyo, jumla ya shilingi bilioni 2.225 zilipatikana kupitia michango na ahadi za wadau mbalimbali kwa ajili ya kuunga mkono Mfuko wa Matibabu ya Upandikizaji wa Figo na Uloto. Fedha hizo zitatumika kusaidia matibabu ya wagonjwa pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma za upandikizaji wa figo na uloto.



