TANGAZO

TANGAZO

RAIS SAMIA ATOA WITO KWA BARA LA AFRIKA KUJITEGEMEA KATIKA MASUALA YA AFYA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuwekeza katika huduma za afya za kibingwa ili kupunguza gharama na utegemezi wa matibabu nje ya Bara hilo.

Rais Dkt. Samia amesema hayo leo tarehe 01 Agosti, 2026, jijini Luanda baada ya kufungua Hospitali ya Rais Julius Nyerere ya Matibabu ya Majeraha ya Moto, akiambatana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço.

Amesema hospitali hiyo ni ushahidi kuwa ndoto ya Angola ya kubadilisha sekta ya afya kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za kisasa za afya ndani ya nchi, inaendelea imetimia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu  Rais pia ameipongeza Angola kwa kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa, ikiwemo matibabu ya majeraha makubwa, majeraha ya moto, macho na maeneo mengine yanayohitaji teknolojia na utaalamu wa kiwango cha juu.

Rais Dkt. Samia amesema uwekezaji huo utaongeza uwezo wa Angola kutibu wananchi wake ndani ya nchi na kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa kupata matibabu nje ya mipaka yake.

Tanzania, amesema Rais Dkt. Samia, imepiga hatua katika matibabu ya huduma za figo, saratani na magonjwa ya moyo, na kwamba Tanzania na Angola zina nafasi kubwa ya kuimarisha ushirikiano katika huduma za kitabibu.

Ameongeza kuwa, ataelekeza wataalamu wa afya kutoka Tanzania kutembelea hospitali hiyo, mahsusi kwa kutibu majeraha yatokanayo na kuungua, kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na wenzao wa Angola.

Vilevile, ametaja ushirikiano wa wataalamu, teknolojia na maarifa kuwa ni muhimu katika kujenga uwezo wa Afrika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake, akieleza kuwa uwekezaji katika huduma za kibingwa ni sehemu ya kujenga uhuru wa kiafya wa Afrika na kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya Bara.

“Waasisi wa Mataifa yetu walipigania uhuru wa nchi zetu ili kuzikomboa kutoka kwenye makucha ya wakoloni. Sisi tuliopo tuna jukumu la kuimarisha uhuru wa kiuchumi, maendeleo na haki za watu wa Afrika,” amesema Rais Dkt. Samia.

Kwa upande wake, Rais João Manuel Gonçalves Lourenço amesema uwepo wa hospitali hiyo nchini Angola, unaziba pengo la matibabu ya kibingwa, hususan kwa waathirika wa majeraha ya moto ambao uhitaji huduma ya haraka.

Rais Lourenço amesema uamuzi wa kuipa hospitali hiyo jina la Mwalimu Nyerere unatambua mchango wa Kiongozi huyo katika kulijenga Taifa lake, na kusaidia ukombozi wa mataifa mengine Barani Afrika.

“Angola ya leo inaendelea kuthamini nafasi ya Mwalimu Nyerere, ambaye nchi yake iliwapokea wapigania uhuru, wanajeshi na raia wakati wa mapambano ya kusaka uhuru wa nchi yetu,” amesema Rais Lourenço.

Halikadhalika, amemshukuru Rais Dkt. Samia, Mama Maria Nyerere na familia ya Mwalimu Nyerere kwa kushiriki ufunguzi huo, akisema uwepo wao umeipa hafla hiyo uzito wa kihistoria.

Amesema kuwa, ingawa Angola imechelewa kutoa heshima hiyo kwa Mwalimu Nyerere, uwepo wa Rais Dkt. Samia na familia ya Baba wa Taifa umeufanya ufunguzi wa hospitali hiyo kuwa wa maana zaidi.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya wa Angola, Dkt. Sílvia Lutucuta amesema Hospitali ya Rais Julius Nyerere imejengwa kuongeza uwezo wa Angola kutoa huduma za kibingwa na matibabu kwa wagonjwa wenye hali ngumu zinazohitaji utaalamu, teknolojia na uangalizi maalumu.

Dkt. Lutucuta amesema hospitali hiyo itakuwa kituo cha utafiti, ubunifu, mafunzo na umahiri wa kitaaluma kwa wataalamu wa afya. Ameongeza kuwa, hospitali imeanza kutoa huduma ikiwa na vitengo maalumu vya tiba ya watoto wachanga, watoto wadogo.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Mwalimu Nyerere, Bw. Madaraka Nyerere ameishukuru Serikali ya Angola kwa kuendeleza urithi wa Mwalimu kupitia taasisi itakayotoa huduma na kuokoa maisha ya wananchi.

Amesema ni matumaini ya familia kuona Hospitali ya Rais Julius Nyerere inakuwa kituo cha ubora katika matibabu, mafunzo na utafiti, huku ikiimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, Rais Dkt. Samia alishiriki hafla ya uzinduzi wa kampeni ya “Building Resilience for Women and Girls: Climate, Conflict and Sustainable Futures," kwa lengo la kuwawezesha wanawake na wasichana kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, migogoro na kujenga mustakabali endelevu.

Rais Dkt. Samia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wenza wa Viongozi wa Afrika kuunga mkono juhudi za kuboresha afya na ustawi wa wananchi wa Bara hilo, hususan katika utekelezaji wa majukumu yake ya U-kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.

Kampeni hiyo iliyoandaliwa pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Wenza wa Viongozi wa Afrika (OASAD) iliwaleta pamoja wenza wa Marais wa nchi za Cabo Verde, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Gabon, Msumbiji, Sierra Leone, Namibia, Nigeria na visiwa vya São Tomé e Príncipe.