Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula, leo Oktoba 17, 2026, amefunga rasmi mafunzo ya awali ya Askari Wanafunzi wa Jeshi la Magereza, Kozi Na. 33, yaliyodumu kwa takribani miezi tisa katika Chuo cha Magereza Kiwira, jijini Mbeya.
Jumla ya askari wanafunzi 1,561 wamehitimu mafunzo hayo, wakiwemo wanawake 367 na wanaume 1,194, kati ya wanafunzi 1,564 walioanza mafunzo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Rwezimula amewataka wahitimu kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uadilifu na nidhamu, kwa kuzingatia sheria na taratibu za Jeshi la Magereza na Taifa kwa ujumla, huku wakitanguliza maslahi ya Jeshi na Taifa. Pia, amewasisitiza kuzingatia tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa hali ya hewa kuhusu mvua za El Nino. Baada ya kukagua gwaride la wahitimu, Dkt. Rwezimula alizindua nyumba tatu za makazi ya askari zenye uwezo wa kuhudumia familia sita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Magereza amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi hilo kupitia ongezeko la bajeti, kuboresha stahiki za watumishi na kutoa vibali vya ajira. Aidha, amesema hivi karibuni Mhe. Rais amewapandisha vyeo maafisa 36, wakiwemo Naibu Makamishna 14 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi 22.
Ameeleza kuwa Jeshi la Magereza limeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi, yakiwemo kutoa hifadhi salama kwa wafungwa kwa mujibu wa sheria, kuendesha programu za urekebishaji, kuzuia uhalifu na kutoa huduma kwa mahabusu. Ameongeza kuwa mafunzo ya Kozi Na. 33 yametumia mitaala mipya inayolenga kuongeza ufanisi wa watumishi katika kutekeleza wa majukumu yao.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Magereza Kiwira, ACP Fred Wambura amesema wahitimu wamepatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali, yakiwemo sayansi ya urekebishaji, ulinzi na usalama wa magereza, usimamizi wa wafungwa, mawasiliano, usimamizi wa rasilimali, maadili ya utumishi na haki za binadamu.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Catherine Afwilile Mwakijungu amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha ajira kilichowawezesha kupata nafasi za kujiunga na Jeshi la Magereza, pamoja na Mkuu wa Jeshi hilo kwa kuwapa nafasi ya kuhudhuria mafunzo yaliyowawezesha kuhitimu hii leo.





