Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inaendelea kuimarisha mikakati madhubuti ya kupambana na VVU na UKIMWI kupitia ushirikiano wa kisekta, kuhamasisha vyanzo vya fedha vya ndani, kusogeza huduma karibu na jamii ikiwemo Vituo vya Maarifa kwa madereva wa malori na kuwajengea uwezo vijana na wanawake ili kufikia lengo la kutokomeza kabisa janga hili ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ilipokutana kwa lengo la kupokea taarifa ya wasilisho la hali ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa Vijana na Mkakati wa Kupunguza Maambukizi Mapya kwa Vijana, kilichofanyika tarehe 20 Agosti, 2026 Bungeni Jijini Dodoma.
Waziri Kabudi ameipongeza Kamati kwa namna ilivyoshauri na kupendekeza uboreshwaji wa masuala mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, kuongeza nguvu kufikia vijana hasa walioko vijijini, elimu zaidi katika maeneo ya starehe ikiwemo kumbi za miziki na makongamano ya vijana lengo ni kuhakikisha jamii inafikiwa kwa ukubwa wake.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt. Johannes Lumbulung Lukumay ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna inavyoratibu masuala ya Afua za UKIMWI nchini huku akieleza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha Utekelezaji wa Afua hizo unafanikiwa bila mkwamo wowote.
“Ni vyema sasa kuendelea kuwajengea uwezo vijana katika mikoa yenye ushamiri mkubwa wa maambukizi na kuratibu utoaji wa elimu na upimaji wa hiari katika maeneo ya kazi na sekta ya usafirishaji hususan kwa madereva wa malori wa masafa marefu," alisema Dkt. Lukumay
Vilevile ameipongeza Serikali kwa namna ilivyowekeza nguvu kuhakikisha janga hili linatokomezwa pamoja na kubuni program na miradi mbalimbali ikiwemo ya TIMIZA Malengo Awamu ya Tatu, inayoendeshwa na kauli mbiu isemayo; "Tusonge na Samia kutokomeza UKIMWI, ambavyo vinaleta mwamko wa jamii kujitokeza kupima afya zao na kuendelea kuchukua tahadhari juu ya maambukizi mapya ya VVU.
Pia wajumbe wa kamati hiyo wamepongeza na kuishukuru Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa Dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) zinazosaidia kuimarisha kinga ya mwili, kuzuika VVU kujizalisha mwilini na kushusha kiwango cha Virusi hadi kutokuonekana ili kuzuia maambukizi mapya kwa jamii.
Akifafanua hoja za wajumbe wa kamati hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Adam Mrisho amesema, ofisi yake imeendelea kuweka mikakati madhubuti na hatua za makusudi katika kuhakikisha utekelezaji wa Afua za UKIMWI unafanyuka vyema na kuyafikia makundi yote hususan vijana.
“Tume imejipanga kuhakikisha elimu inaendelea kuifikia jamii ili kuwa na utayari wa kupima na kuhamasisha matumizi ya dawa kwa watakao gundulika kuwa na maambukizi ya VVU pamoja na kuimarisha mashirikiano na sekta binafsi” alieleza Dkt. Mrisho
Jitihada zingine ni kuwezesha wahudumu ngazi ya jamii wapatao elfu tisini kwa kuwapatia elimu ya kutoa huduma za kinga na huduma za JIPIME, hivyo kusaidia kuwafikia vijana waliopo vijijini na kuongeza mwitikio wa masuala ya UKIMWI.
Pia mikakati mingine ni kuviwezesha na kuboresha vituo 32 vya maarifa vinavyotoa elimu ya kinga, huduma za ARVs, upimaji na kuhakikisha vijana wanapewa elimu za masuala ya UKIMWI hususani madereva wa malori ya masafa marefu kupitia vituo hivyo vilivyopo nchini.


