Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Tanzania nchini Malaysia, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, Mazungumzo yaliyofanyika mkoani Dodoma, leo tarehe 20 Agosti 2026.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amempongeza Balozi Mkeremy kwa imani aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kuliwakilisha Taifa katika nchi ya Malaysia. Amesema nchi hiyo yenye uchumi mkubwa, ina ushirikiano wa kimkakati na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya kibiashara na majukwaa ya kimataifa.
Makamu wa Rais amemsihi Balozi Mkeremy kufanya kazi kwa jitihada na ubunifu kuhakikisha anaimarisha zaidi urafiki wa Tanzania na Malaysia kwa kuongeza fursa na kukaribisha wawekezaji wengi zaidi nchini. Pia, amemsisitiza kuhamasisha watanzania waishio Malaysia (Diaspora) kuwekeza nchini Tanzania.
Amemsihi Balozi Mkeremy kufahamu vema Dira ya Taifa 2050 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2025 – 2030 ili kutambua mambo ya uhusiano wa kimataifa yaliyopewa kipaumbele na yanayohitaji msisitizo wa kipekee kuyatekeleza.
Kwa upande wake Balozi mteule wa Tanzania nchini Malaysia, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwakilisha Taifa nchini Malaysia. Aidha, amemshukuru Mhe. Makamu wa Rais kwa nasaha zake na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.


