TANGAZO

TANGAZO

WIZARA YA MADINI YAFUMUA SOKO LA MADINI LISILO RASMI DAR ES SALAAM NA KUKAMATA WAHUSIKA




Wizara ya Madini imefanikiwa kufanya oparesheni maalumu ya kuwasaka wafadhili na wawezeshaji wa wanunuzi wa madini wanaofanya biashara hiyo nje ya mfumo wa masoko yaliyoidhinishwa na Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 9,2026 katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde amesema oparesheni hiyo ni utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa tarehe 27 Julai, 2026 katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Amesema maelekezo hayo yalitolewa baada ya Serikali kukamata madini ya dhahabu yaliyokuwa yakitoroshwa nje ya nchi.

“maagizo kwa kikosi kazi kuhakikisha kinawakamata wale wanaowafadhili watoroshwaji wa madini. Tulitaka kujua madini haya yaliyokamatwa mikoani yanaishia wapi na yanauzwa na nani,” alisema Waziri Mavunde.

Waziri Mavunde amebainisha kuwa kupitia oparesheni hiyo, Wizara imefanikiwa kubaini kuwepo kwa soko la madini lisilo rasmi katika eneo la Mtaa wa Jamhuri, jijini Dar es Salaam, katika jengo moja la ghorofa tano.

Ameeleza kuwa imekuwa ni desturi kwa wachimbaji wadogo kutoka mikoa mbalimbali kwenda kuuza madini katika eneo hilo, badala ya kuyapeleka katika masoko rasmi yaliyotambuliwa na Serikali.

“Eneo hilo kwa sasa liko chini ya ulinzi na wahusika wote wamekamatwa. Hata hivyo kwa kuwa ni eneo la makazi na linahusisha watu wasio na hatia, tumeona si vema kufanyia mkutano na waandishi wa habari pale. Tungeweza kuwaathiri watu wengine wasio husika. Ndio maana tumetoa taarifa hii hapa ofisini,” aliongeza Waziri.

Vitu vilivyokamatwa ni Madini gram 174 yaliyokutwa katika soko hilo bubu pamoja na   mashine mbili za XRF aina ya NITON DXL 800, Mizani ya kupimia uzito, Mitungi ya gas, vyungu vya kuchomea dhahabu, borax, pipeza gas, legis za kutengenezea umbo la dhahabu Pamoja na jumla ya pesa taslimu TZS. 54,705,000 vyote vinashikiliwa na serikali.

Wizara imeahidi kuendelea na msako mkali dhidi ya mitandao yote inayojihusisha na ununuzi na utoroshaji wa madini nje ya mfumo.