TANGAZO

TANGAZO

KIRUSWA: MSAADA WA KIUFUNDI NI CHACHU YA KUONGEZA TIJA UCHIMBAJI MDOGO WA MADINI

 



Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za mwaka 2025, akieleza kuwa kanuni hizo ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija, usalama na ufanisi wa shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini.









Dkt. Kiruswa ameyasema hayo mapema leo mkoani Geita wakati akizungumza katika warsha iliyolenga kujadili na kutoa uelewa wa kina kuhusu kanuni hizo, ambapo amesema Serikali inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata teknolojia, mitambo, ujuzi na utaalamu wa kisasa ili kuboresha shughuli zao za uchimbaji na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.


Amesema kwa muda mrefu wachimbaji wadogo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za mitaji, teknolojia na utaalamu, hali ambayo imekuwa ikiathiri tija na ufanisi wa shughuli zao.


Kwa kutambua changamoto hizo, amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kupata msaada wa kiufundi kutoka kwa wataalamu na wadau wenye uwezo, ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia misingi ya kitaalamu na kibiashara.


Kwa mujibu wa Dkt. Kiruswa, msaada wa kiufundi unapaswa kujikita katika maeneo muhimu ikiwemo utafiti wa kijiolojia, usanifu wa migodi, teknolojia za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, usalama na afya migodini, utunzaji wa mazingira, pamoja na usimamizi wa fedha na biashara.


Amesisitiza kuwa utekelezaji wa kanuni hizo unapaswa kuleta matokeo yatakayomwezesha mchimbaji mdogo wa madini kufanya maamuzi ya uwekezaji kwa kuzingatia taarifa za kitaalamu, kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa rasilimali za madini.


Aidha, amewataka wamiliki wa leseni za madini na watoa huduma za msaada wa kiufundi kutumia warsha hiyo kujenga uelewa wa pamoja kuhusu kanuni hizo na kuhakikisha mikataba ya msaada wa kiufundi inaandaliwa na kutekelezwa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni za nchi.


Dkt. Kiruswa amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, kutumia wataalamu wenye sifa, kuimarisha usalama na afya kazini, kutunza mazingira na kuzingatia misingi ya nidhamu ya biashara.


“Matarajio ya Serikali ni kuona mchimbaji mdogo wa leo anakua na kuwa mchimbaji wa kati, na hatimaye kuwa kampuni kubwa ya Kitanzania yenye uwezo wa kushindana ndani na nje ya nchi,” amesema.


Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, amesema Wizara ya Madini imeweka kanuni hizo kwa lengo la kulinda maslahi ya makundi yote yanayohusika katika utekelezaji wa msaada wa kiufundi.


Amesema Serikali ipo tayari kupokea na kufanyia kazi maoni na mapendekezo yatakayotolewa na washiriki wa warsha hiyo, ili kuendelea kuboresha utekelezaji wa kanuni hizo.


“Wizara ipo kwa ajili ya kujenga na kuweka mazingira yatakayowezesha shughuli za uchimbaji kuendelea kwa manufaa ya wahusika wote,” amesema.


Aidha, amewapongeza wadau na wageni wanaoshirikiana na kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia utaalamu, teknolojia na uzoefu unaohitajika katika kuboresha shughuli zao za uchimbaji.


Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, amesema warsha hiyo inalenga kujenga uelewa wa wadau kuhusu masuala ya kiufundi katika shughuli za uchimbaji madini, pamoja na kuwawezesha wazawa kutumia ipasavyo utaalamu, teknolojia na maarifa yanayotolewa kupitia msaada wa kiufundi.


Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwezo wa wachimbaji wadogo katika kuboresha shughuli zao, kuongeza tija na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya usalama na utunzaji wa mazingira.